Siku ya Watu wa Amerika ya Kusini: lengo kukuza na kuimarisha umoja, mshikamano katika
Uinjilishaji Mpya!
Kunako mwako 1959 Kanisa lilianzisha Siku ya Watu wa Amerika ya Kusini, inayoadhimishwa
kila Mwaka ifikapo tarehe 3 Machi. Lengo ni kukuza na kuendeleza mchakato wa umoja,
mshikamano na ushirikiano katika Uinjilishaji, kati ya Hispania na Nchi za Amerika
ya Kusini.
Katika maadhimisho
ya Mwaka wa Imani uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi
na sita, sanjari na Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa
Vatican, waamini wanaoishi Amerika ya Kusini wanakumbushwa kwamba, hili ni eneo ambalo
malango yake yako wazi kwa ajili ya Uinjilishaji.
Ni mwaliko kwa kila mwamini
kukumbuka ile dhamana ya kutangaza Injili ya Kristo kwa njia ya ushuhuda wa maisha
yake pamoja na kushiriki katika kuendeleza harakati za kimissionari sehemu mbali mbali
za dunia, kwani wakumbuke daima kwamba, ni upendo wa Kristo unaowasukuma Kuinjilisha.
Haya ni maneno ya Kardinali Marc Ouellet, Rais wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya Amerika
ya Kusini katika ujumbe wake kwa Maadhimisho haya. Juhudi za kimissionari ni kigezo
muhimu sana kinachoonesha uhai wa Kanisa na Jumuiya zake za Kikristo.
Takwimu
zinaonesha kwamba, walau asilimia 50% ya Waamini wa Kanisa Katoliki wanaishi Amerika
ya Kuini. Hii ndiyo imani ambayo imepelekea Kanisa Katoliki kuwa na idadi kubwa ya
Mapadre na Watawa kutoka Amerika ya Kusini, utume na dhamana iliyofanywa na wadau
mbali mbali wa Injili kutoka Hispania. Juhudi za Uinjilishaji mpya anasema Kardinali
Ouellet zinajikita hasa zaidi katika toba na wongofu wa ndani, ili kuweza kukabiliana
na changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo
ya sayansi na teknolojia.
Kuna mabadiliko makubwa yanayogusa medani mbali
mbali za maisha ya mwanadamu; Njia za mawasiliano ya Kijamii zimekuwa ni majukwaa
mengine yanayopaswa Kuinjilishwa ili yaweze kukumbatia kweli za Kiinjili na tunu bora
za maisha na utu wa mwanadamu.
Maendeleo haya pia yameibua kundi kubwa la maskini
na watu wasiokuwa na ajira, hali ambayo inaendelea kusababisha shida na mahangaiko
makubwa ya watu sehemu mbali mbali za dunia, hususan kwenye miji mikubwa. Kuna wazee
waliokata tamaa, wasiokuwa na matumaini tena kutokana na kupanda kwa gharama za maisha
na kushuka kwa hali ya maisha; ni watu wanaokosa huduma msingi za tiba na malazi;
hao ndio wanaoteseka na baridi pamoja na joto katika mitaa ya miji mikubwa duniani.
Kumekuwepo na ongezeko la nyanyaso kwa wanawake na wasichana, hali inayowatumbukiza
hata katika utumwa mamboleo.
Kutokana na kukabiliana na hali ngumu ya maisha,
vijana wengi wamejikuta wakijitumbukiza katika matumizi haramu ya dawa za kulevya
na ulevi wa kupindukia pamoja makosa ya jinai. Kundi la vijana wasiokuwa na fursa
za ajira ni hatari kwa maisha, ustawi na maendeleo ya Jamii, kwani wanaweza kutumiwa
na watu wasiokuwa na nia njema kuleta machafuko kama inavyojionesha sehemu mbali mbali
za dunia.
Kardinali Marc Ouellet anasema licha ya kundi kubwa la wananchi kutopea
katika umaskini wa kipato na kihali, lakini kuna baadhi ya watu wanaoendelea kuponda
maisha, huku “wakila kuku kwa mirija”! Ni watu wanaojibovusha kwa starehe na anasa
pamoja na kuendelea kuzama katika wimbi la mmong’onyoko wa kimaadili na utu wema.
Mazingira kama haya yanaendelea kuhatarisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia,
kiasi kwamba, watu wanaanza kujikuta wakikimbatia utamaduni wa kifo, unaowaacha watoto
na vijana wakiwa yatima; wakikosa malezi bora na makini kutoka kwa wazazi na walezi
wao! Hawana mifano bora ya kuigwambele yao!
Utepetevu wa imani, maadili na
utu wema ni mwaliko na changamoto ya pekee katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, kutubu
na kuongoka, ili waamini waweze kuwa kweli ni wafuasi amini wa Kkristo kwa maneno,
lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa matendo yao yanayoonesha ile imani tendaji na
kwa njia hii, watu wengi wataweza kumfahamu tena Kristo.
Toba na wongofu wa
ndani uguse mihimiri ya shughuli na mikakati ya shughuli za kichungaji sanjari na
kuamsha tena ari na moyo wa kimissionari ili kuweza kuwashirikisha wengine ile furaha
ya kukutana na Yesu katika Maandiko Matakatifu, Maisha ya Kisakramenti na Matendo
ya Huruma. Waamini wajenge moyo wa upendo na mshikamano na wote wanaosukumizwa pembezoni
mwa Jamii na kwa namna ya pekee wahamiaji na wageni.
Vyama vya kitume viendelee
kutekeleza wajibu na majukumu yao ya kila siku kwa, kwa kuwashirikisha waamini walei
ambao wanadhamana nyeti ya kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda amini wa
maisha yao kwa Kristo na Kanisa lake. Watawa na Makleri washirikiane kwa karibu zaidi
na waamini walei katika utekelezaji wa dhamana na utume wa Kanisa katika Uinjilishaji
Mpya.
Kardinali Marc Ouellet, Rais wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya Amerika
ya Kusini anahitimisha ujumbe wake kwa kuwataka waamini wote kushirikiana kwa na kujitoa
bila ya kujibakiza katika maisha na utume wa Kanisa.