"Mimi si Khalifa wa Mtakatifu Petro tena! Bali Hujaji anayeanza hatua ya mwisho ya
hija ya maisha yake hapa duniani"
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kabla ya kung'atuka rasmi kutoka madarakani
hapo tarehe 28 Februari 2013, saa 2:00 Usiku, alipata fursa ya kusalimiana na waamini,
mahujaji na wageni waliokuwa wamefurika kwa wingi kwenye Viunga vya Ikulu Ndogo ya
Castel Gandolfo, nje kidogo ya mji wa Roma. Baba Mtakatifu alitokeza kwenye dirisha
na kuwashukuru wote kwa upendo na mshikamano wanaomwonesha, ingawa wakati huu kuna
hali tofauti kabisa na siku nyingine zilizotangulia.
Kwa unyenyekevu mkubwa,
Baba Mtakatifu amesema, kuanzia saa 2: 00 Usiku, hatakuwa tena Khalifa wa Mtakatifu
Petro, bali hujaji anayeanza hatua ya mwisho wa maisha yake hapa duniani. Anasema
kwa: moyo,upendo, sala, tafakari na nguvu zilizoko ndani mwake, kuendelea kufanya
kazi kwa ajili ya mafao ya Kanisa na Ulimwengu kwa ujumla. Anawaalika waamini na wote
wenye mapenzi mema, kushikamana kwa dhati na Kristo kwa ajili ya mafao na ustawi wa
Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake.
Mwishoni, Baba Mtakatifu Benedikto
wa kumi na sita, aliwapatia baraka zake za kitume na hatimaye kurejea ndani. Huu ukawa
ni mwisho kwa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kuonekana hadharani kama Khalifa
wa Mtakatifu Petro.