2013-03-01 10:35:56

Kiti cha ukulu wa Mtakatifu Petro kiko wazi!


Baada ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kuamua kung'atuka kutoka madarakani, baada ya kuliongoza Kanisa kwa kipindi cha miaka minane, sasa kiti cha Ukulu wa Mtakatifu Petro kiko wazi. Kama Familia ya Wasalesiani wa Mtakatifu Bosco, wanatambua na kuthamini mchango wa Papa Benedikto wa kumi na sita, mwaliko wa kuendelea kusali kwa ajili yake.

Ni maneno ya Mheshimiwa Padre Pascual Chavez, Mkuu wa Shirika la Wasalesiani, anayemshukuru Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, ambaye amekuwa kweli ni zawadi kubwa ya Mungu kwa Kanisa na Ulimwengu kwa ujumla. Ameonja ukarimu na uwepo wa Familia ya Mungu, hata pale ambapo watu walidhani kwamba, "Mungu anasinzia". Wasalesiani wanapenda kumhakikishia Baba Mtakatifu mstaafu uwepo wao wa karibu kwani Mafundisho yake yataendelea kuhifadhiwa katika sakafu za mioyo yao!

Kwa wakati wake, historia itatoa hukumu ya maisha na utume wa Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto wa kumi na sita kwa kuonesha ukuu wa binadamu, akili na maisha thabiti ya kiroho. Upendo wake kwa Kristo na Kanisa lake, utaendelea kung'ara miongoni mwa Familia ya Mungu na kwamba, amejitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kulihudumia Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake. Yeye mwenyewe anawakumbusha waamini kwamba, Kanisa haliwezi kubaki kama mtoto yatima kwani, Kristo ni kichwa cha Kanisa linaloongozwa kwa nguvu za Roho Mtakatifu.

Wasalesiani wanaalikwa kuungana na Kanisa zima kwa ajili ya kusali ili kuombea mchakato wa uchaguzi wa Papa Mpya, kadiri ya mpango wake. Katika kipindi cha Kwaresima, toba na wongofu wa ndani ni mambo yanayopaswa kupewa msukumo wa pekee, ndivyo Mheshimiwa Padre Pascual Chàvez, Mkuu wa Shirika la Wasalesiani wa Don Bosco anavyohitimisha ujumbe wake kwa ajili ya kumwombea Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita pamoja na kuombea mchakato wa uchaguzi wa Papa mpya!







All the contents on this site are copyrighted ©.