2013-02-28 15:07:21

Yaliyojiri wakati wa Papa kukutana na Makardinali


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Alhamisi, tarehe 28 Februari 2013 amekutana na kusalimiana na Makardinali 144 ambao tayari wako mjini Vatican kushiriki katika mchakato wa kumchagua Papa mpya baada ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kung'atuka rasmi kutoka madarakani, tarehe 28 Februari 2013, saa 2:00 Usiku, tukio ambalo litarushwa moja kwa moja kutoka Castel Gandolfo.

Baba Mtakatifu pia amepata fursa ya kukutana na kusalimiana na viongozi waandamizi kutoka Mabaraza ya Kipapa, Washereheshaji na baadhi ya Wafanyakazi kutoka Sekretarieti ya Vatican ambao kwa takribani miaka minane wamefanya naye kazi bega kwa bega. Baba Mtakatifu katika hotuba yake ya mwisho kwa Makardinali amefafanua maana ya Kanisa, dhana ambayo Baba Mtakatifu mwenyewe alijitahidi kuiishi katika utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Baba Mtakatifu amewakumbusha Makardinali kwamba, kati yao kulikuwemo Papa Mpya, ambaye tangu wakati huu anaahidi kumpatia heshima na utii mkamilifu. Huu ni mwelekeo ambao Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita amependa kuuonesha kwa Makardinali hata kabla ya kukamilika mchakato wa uchaguzi wa Papa Mpya, uchaguzi ambao kimsingi hatahusika hata kidogo.

Kardinali Angelo Sodano, Dekano wa Makardinali amewaambia Makardinali kwamba, tarehe Mosi, Machi, atawatumia rasmi barua za mwaliko wa kushiriki kwenye mkutano wa Dekania ya Makardinali wenye dhamana ya kumchagua Papa Mpya. Makardinali watashiriki katika mkutano huu kwa kufuata umri na mwaka walioteuliwa kuwa Makardinali na baadaye watafuata Madaraja yao; yaani: Makardinali Maaskofu ambao wamepangia utume katika Makanisa makuu yaliyoko Jimbo kuu la Roma.

Kuna Makardinali Mapadre, hawa ni wale waliopangiwa utume kwenye Parokia za Jimbo kuu la Roma, hawa ni Maaskofu wakuu wa Majimbo makuu kutoka sehemu mbali za dunia. Mwishoni, kuna Makardinali Mashemasi wanaotekeleza utume wao ndani ya Vatican kama wakuu wa Mabaraza ya Kipapa.

Ufafanuzi huu umetolewa na Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican. Anabainisha kwamba, kuna jumla ya waandishi wa habari 3,641, wanaozungumza lugha 24 kutoka katika mataifa 61. Baadhi ya waandishi wa habari ni wale ambao wamesajiliwa kwa muda.







All the contents on this site are copyrighted ©.