2013-02-28 11:05:04

Wanawake Wakatoliki wanamshukuru Baba Mtakatifu Benedikto XVI kwa kusimama kidete kulinda na kutetea wito wa wanawake katika Kanisa na Jamii


Wanawake wana mchango mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa kama ilivyo hata katika Jamii. Wanawake wanapaswa kuwa waaminifu kwa mpango wa Mungu, utu na heshima yao, daima wakijikita katika haki na usawa na kukataa katu katu aina zote za nyanyaso dhidi ya wanawake.

Ni maneno ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita katika nyaraka zake za kichungaji ambayo yanatumiwa wakati huu na Shirikisho la Vyama vya Wanawake Wakatoliki kumshukuru Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwa kuwatia shime kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa.

Wanawake Wakatoliki wanaahidi kuendelea kumwombea Baba Mtakatifu anapoanza maisha mapya baada ya kuliongoza Kanisa kwa miaka minane. Wanamshukuru kwa kuwachangamotisha kutangaza Injili ya Kristo sanjari na kugundua hazina ya imani kwa kuitolea ushuhuda amini.

Wanawake kwa unyenyekevu mkuu wanamwomba Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kuwakumbuka katika sala zake, wanapoendelea kujibidisha katika utekelezaji wa mchakato wa Uinjilishaji mpya sehemu mbali mbali za dunia kwa kushirikisha wito na karama walizokirimiwa na Mwenyezi Mungu. Wanamwombea amani na utulivu wakati huu anapoanza ukurasa mpya wa maisha yake!







All the contents on this site are copyrighted ©.