2013-02-28 08:59:06

Salini zaidi ili kumwomba Roho Mtakatifu aweze kulijalia Kanisa Papa Mpya!


Waamini wanaalikwa kusali kwa nguvu zaidi kwa kumwomba Roho Mtakatifu ili aweze kulijalia Kanisa Baba Mtakatifu Mpya, atakayeliongoza Kanisa, akiwa ni kielelezo cha umoja, mshikamano na upendo miongoni mwa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Kiongozi makini atakayesimamia imani, maadili na utu wema, mambo msingi katika maisha na utume wa Kanisa. Kanisa linahitaji kiongozi atakayewasaidia waamini kuendelea kukua na kukomaa katika misingi ya imani, matumaini na mapendo. RealAudioMP3

Ni maneno ya Askofu Damian Dallu wa Jimbo Katoliki Geita, Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican, wakati huu Kanisa linapoendelea kutafakari uamuzi wa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kung'atuka kutoka madarakani na hivyo kutoa fursa kwa Makardinali kuanza mchakato wa kumtafuta Papa Mpya. Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwa hakika atakuwa ni mfano na kielelezo cha jinsi ya kuachiana dhamana ya kuliongoza Kanisa ambalo ni mali ya Kristo mwenyewe!

Askofu Dalli anawaalika waamini na watu wenye mapenzi mema kulipokea tukio hili kwa imani, matumaini na mapendo na kwamba, kwa njia ya Kanisa watu wengi waweze kupata maisha ya uzima wa milele, kwa kuendelea kuenzi urithi wa imani na mafundisho ya Kanisa. Waamini wajitahidi kuwa kweli ni mashahidi amini wa Kristo, ili kuendelea kuwavuta wengi zaidi waweze kumfahamu, kumpenda na kumtumikia na mwisho waweze kupata uzima wa milele.

Mateso na mahangaiko wanayokumbana nayo katika hija ya maisha yao ya kiimani iwe ni chachu ya maandalizi ya kina ili kuweza kushiriki kwa ukamilifu zaidi Fumbo la Pasaka, yaani, mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Waamini wanaalikwa kutumia vyema Kipindi cha Kwaresima sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Imani kujibidisha zaidi katika maisha ya kiroho; kwa kumshukuru Mungu kwa wema na ukarimu wake kwa Kanisa katika kipindi cha Miaka 8 ya Uongozi wa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita.

Ni fursa pia ya kumshukuru Baba Mtakatifu aliyejitoa kimaso maso kulitumikia Kanisa la Kristo. Sasa ni wakati wa kusali zaidi kwa ajili ya kuliombea Kanisa liweze kumpata Papa Mpya kadiri ya mpango wa Mungu.







All the contents on this site are copyrighted ©.