Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Alhamisi tarehe 28 Februari 2013 amekutana
na kuzungumza na Makardinali kwa pamoja na baadaye, Makardinali walipata nafasi ya
kuzungumza na Baba Mtakatifu mmoja mmoja kama alama ya kuagana naye! Baba Mtakatifu
anawashukuru Makardinali kwa kufanya hija pamoja naye katika kipindi cha miaka minane,
kwa pamoja wakitembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka.
Anawashukuru kwa mawazo
na ushauri waliompatia wakati alipokuwa anatekeleza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu
Petro na kwamba, katika kipindi cha miaka minane kwa pamoja wamefanya hija ya imani,
kwa kutembea katika mwanga wa Kanisa, ingawa wakati fulani, kulikuwepo na wingu zito
lililotanda kiasi cha kutishia maisha na utume wa Kanisa. Kwa pamoja wamejitahidi
kulihudumia Kanisa la Kristo kwa imani, mapendo na sadaka kubwa; kwa kuwashirikisha
waamini matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo, wakakua na kukomaa katika umoja
na mshikamano.
Baba Mtakatifu anawaomba Makardinali kushikamana katika utofauti
wao, daima wakitamani kulitumikia Kanisa la Kristo, kwa kutambua kwamba, Kanisa ni
Fumbo la Mwili wa Kristo, linalowashirikisha waamini wote katika ujumla wao, Kanisa
ni hali halisi inayojionesha katika uhalisia wa maisha na moyo wa Kanisa ni Yesu mwenyewe
na linaongozwa na nguvu ya Roho Mtakatifu. Liko duniani lakini si la dunia kwani Kanisa
ni mali ya Fumbo la Utatu Mtakatifu.
Kanisa linaendelea kukua na kukomaa ili
kuamsha roho za watu, kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria kuweza kulipokea Neno la Mungu
kadiri ya uwezo wa Roho Mtakatifu kwa kujitoa kikamilifu ili kupokea mpango wa Mungu,
katika hali ya unyenyekevu na ufukara katika mchakato wa kumpeleka Kristo kwa watu!
Baba Mtakatifu anawataka Makardinali kushikamana katika Fumbo la Maisha na Utume wa
Kanisa; kwa sala, lakini zaidi katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, kama
kielelezo cha huduma kwa Kanisa na Ulimwengu kwa ujumla.
Baba Mtakatifu amewahakikishia
Makardinali kwamba, ataendelea kuwa karibu nao kwa njia ya Sala, hasa wakati huu wanapojiandaa
kumchagua Papa Mpya, ili kuweza kusikiliza sauti ya Roho Mtakatifu kwa ajili ya Kanisa
lake. Baba Mtakatifu anasema, atakuwa mwaminifu na mtiifu kwa Papa mpya!