Baraza la Makanisa Ulimwenguni lina mshukuru Papa Benedikto XVI
Dr. OLav Fyske Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC, amemwandikia
barua ya shukrani Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kumshukuru kutokana na
mchango wake mkubwa katika kukuza na kukoleza majadiliano ya kiekumene miongoni mwa
wafuasi wa Kristo. Baraza la Makanisa linamtakia kila la kheri katika maisha yake
mapya ya sala na tafakari ya kina.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita,
tangu mwaka 1971 akiwa Jaalim wa Taalimungu, alitoa mchango mkubwa katika majadiliano
ya kiekumene, ari ambayo ameiendeleza kwa kasi mpya hata baada ya kuchaguliwa kuliongoza
Kanisa Katoliki katika kipindi cha miaka minane. Umoja wa Kanisa unaofumbata pia umoja
wa Familia ya binadamu anasema, Dr. Tveit.
Baraza la Makanisa Ulimwenguni linamshukuru
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kwa mchango wake mkubwa wa hali na mali katika
kuhimiza majadiliano ya kiekumene, kwa kukazia zaidi ushuhuda wa pamoja katika kulinda
na kutetea haki msingi za binadamu, utu na maadili mema sanjari na kujenga misingi
ya amani na utulivu, kama ilivyojionesha wakati wa Kumbu kumbu ya Jubilee ya miaka
25 tangu Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili alipoitisha mkutano wa viongozi wa kidini
kwa ajili ya kuombea amani duniani Mjini Assisi, Italia, kunako mwaka 2011. Mazungumzo
ya viongozi hawa wawili kwa wakati huo, ilikuwa ni fursa ya kukuza na kudumisha umoja
na mshikamano katika imani.