Yesu anaendelea hata leo hii kujenga na kuliimarisha Kanisa lake juu ya Mtakatifu
Petro, Mwamba wa Kanisa, ambao kamwe hautaweza kushindwa na nguvu za kuzimu. Mwamba
ulitumika sana katika ibada za Wapagani, lakini mwamba huu unapata maana mpya. Yesu
alipofika pande za Kaisaria Filipi, aliwauliza wanafunzi wake, “watu wanasema kuwa
ni nani?” Wakamjibu wengine wanasema kuwa ni Yohane Mbatizaji, wengine Elia, wengine
Yeremia au mmojawapo wa Manabii.
Yesu akawauliza “Ninyi, Je, mnasema mimi ni
nani?” Simoni Petro akajibu “Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai” Yesu akasema,
“Heri wewe Simoni mwana wa Yona, kwa maana hakuna binadamu yeyote aliyekufunuliajambo
hili, ila Baba yangu aliye mbinguni. Nami ninakuambia wewe ni Petro, na juu ya mwamba
huu nitalijenga Kanisa langu; wala nguvu za kifo hazitaweza kulishinda. Nitakupa funguo
za ufalme wa mbinguni; kila utakachofunga duniani, kitafungwa pia mbinguni; kile utakachofungua
duniani, kitafunguliwa pia mbinguni. Mt. 16:13-19.
Padre Francesco Rossi de
Gasper mtaalam wa Maandiko Matakatifu anasema, Kanisa la Kristo linachangamotishwa
kutangaza Habari Njema ya Wokovu inayojikita kwa Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na
kufufuka kutoka katika wafu, ili kuishi kwao kuwa ni ushuhuda wa Mungu anayeishi na
kutenda kazi ndani mwao. Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anawaalika waamini
na wote wenye mapenzi mema, kumfuasa Kristo wakiongozwa na Injili kama dir ana mwongozo
wa maisha ya kila siku; daima wakiwa tayari kumwachia Mungu nafasi ya kuwaunda kadiri
ya mpango wake, changamoto kwa waamini kufanya maamuzi yao mintarafu mwanga wa Injili.
Baba Mtakatifu anaendelea kusema, leo hii Wakristo hata kama amezaliwa, akaishi
na kuelimishwa katika Jamii na Familia ya Kikristo, lakini hana budi kutoa nafasi
ya kwanza kwa uwepo wa Mungu katika maisha yake, kama sehemu ya mchakato wa kupambana
na vishawishi katika ulimwengu wa utandawazi.
Khalifa wa Mtakatifu Petro, anawaalika
wale ambao wamepokea Mafundisho ya Kikristo, lakini bado hayajazamisha mizizi yake
katika imani au pengine wamekengeuka, kuanza hija ya kumtafuta Yesu Kristo na Injili
yake, kwa kujiandaa kutoka katika undani wa maisha kumkaribisha Mwenyezi mungu anayetaka
kufanya makao katika moyo wa mwanadamu. Kutokana na ukweli huu, waamini hawana budi
kuwa makini kiasi kwamba, hawachafuliwi na ndoto za mchana, mmwonekano wa nje au mali
ya dunia hii.