2013-02-27 08:48:24

Dumisheni haki, amani na utulivu wakati wa mchakato wa uchaguzi mkuu nchini Kenya


Askofu mkuu Boniface Lele wa Jimbo kuu la Mombasa, anawaalika waamini na wananchi wa Kenya katika ujumla wao kuhakikisha kwamba, wanadumisha amani, kabla, wakati na baada ya mchakato wa uchaguzi mkuu nchini humo unaotarajiwa kufanyika hapo tarehe 4 Machi 2013. Hii ni dhamana nyeti kwa ajili ya mafao na ustawi wa wananchi wa Kenya, changamoto ya kuvuka: udini, ukabila na umajimbo ambao unatumiwa na baadhi ya wanasiasa kwa ajili ya kujitafutia umaarufu wakati wa uchaguzi.

Askofu Mkuu Boniface Lele anawahimiza waamini kwa namna ya pekee kabisa kumwilisha ndani mwao ile amri ya upendo kwa Mungu na jirani na kamwe wasiwe ni chanzo cha vurugu na machafuko ambayo yanasababisha maafa makubwa kwa watu wasiokuwa na hatia.

Wananchi wajiandae kupokea kwa unyofu yule ambaye ataibuka kidedea katika kinyang'anyiro cha uchaguzi mkuu nchini humo na kumkubali na kumheshimu, ili aweze kuwatumikia wananchi wote wa Kenya pasi na ubaguzi wala upendeleo. Kenya ni nchi ambayo inaundwa na watu kutoka katika makabila mbali mbali. Kampeni za kikabila anasema Askofu mkuu Boniface Lele hazina tija wala mafao kwa maendeleo ya wananchi wa Kenya, kila mwananchi apewe atumie uhuru wake kikamilifu kumchagua kiongozi anayefaa!

Kasoro ndogo ndogo haziwezi kukosekana katika mchakato wa uchaguzi mkuu, kumbe, kuna haja kwa viongozi watakaokuwa na pingamizi kuhusiana na masuala ya uchaguzi kutumia mkondo wa sheria badala ya kuleta vurugu na uvunjifu wa misingi ya haki, amani na utulivu. Hili ni jambo ambalo kamwe haliwezi kukubalika!







All the contents on this site are copyrighted ©.