2013-02-27 08:28:15

Ataitwa "Baba Mtakatifu mstaafu"


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita baada ya kung'atuka rasmi madarakani hapo tarehe 28 Februari 2013, saa 2:00 Usiku ataanza kuitwa "Baba Mtakatifu Mstaafu". Ufafanuzi huu umetolewa na Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican baada ya wanasheria wa Kanisa kukaa na kulitafakari tukio hili la kihistoria katika maisha na utume wa Kanisa.

Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro tayari umesheheni waamini, mahujaji na watu wenye mapenzi mema kutoka sehemu mbali mbali za dunia waliofika kutoka heshima zao za mwisho kwa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Ratiba inaonesha kwamba, Alhamisi, tarehe 28 Februari 2013, Majira ya asubuhi, Baba Mtakatifu anatarajiwa kukutana na Makardinali ambao wamekwisha wasili hapa mjini Roma kwa ajili ya mazungumzo ya faragha. Jioni ataagwa rasmi na Vikosi vya Ulinzi na Usalama mjini Vatican. Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican ataongoza ujumbe wa viongozi waandamizi kutoka Vatican watakaomuaga Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kabla ya kuondoka rasmi mjini Vatican kuelekea kwenye Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo, nje kidogo ya mji wa Roma.

Baba Mtakatifu anatarajiwa kufika jioni mjini Castel Gandolfo, na huko atapokelewa na Kardinali Giuseppe Bertello, Gavana wa Mji wa Vatican pamoja na Askofu mkuu Giuseppe Sciacca, katibu mkuu wa Gavana wa Vatican, Askofu Marcello Semeraro wa Jimbo la Albano pamoja na viongozi wa Serikali. Atakapo wasili Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo, Baba Mtakatifu atatokeza dirishani kusalimiana na wananchi pamoja na wageni watakaokuwa wamefika mjini Albano. Saa 2:00 Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, atakuwa anang'atuka rasmi kutoka madarakani na tangu wakati huo Kiti cha Ukulu wa Mtakatifu Petro kitakuwa wazi.

Walinzi wa kutoka kutoka Uswiss ambao wamepewa dhamana maalum ya kumlinda Khalifa wa Mtakatifu Petro, kadiri ya Mapokeo ya Kanisa, watakuwa wamemaliza utume wao na kurudi makao makuu ya Vikosi hivi mjini Vatican. Vikosi vya ulinzi na usalama kutoka Vatican vitaendelea kushughulikia masuala ya ulinzi na usalama wa Papa mstaafu. Tangu wakati huo, Baba Mtakatifu hatavaa tena ile "Pete ya Mvuvi" inayoonesha ukulu wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro wala hata vaa tena vile viatu vyekundu alama ya ushuhuda wa imani hata ikibidi kumwaga damu!

Padre Lombardi anasema kwamba, mwanzo mwa Mwezi Machi, Dekano wa Makardinali, atatuma barua ya mwaliko kwa Makardinali wote ili kushiriki katika Mkutano wa Dekania ya Makardinali utakaokuwa na dhamana ya kuanza mchakato wa uchaguzi wa Papa Mpya. Mikutano ya Makardinali inatarajiwa pia kuanza Juma lijalo. Mikutano hii itafanyika kwenye Ukumbi Mpya wa Sinodi.

Kutokana na sababu za kiufundi, Padre Lombardi anasema, Makardinali watahamia kwenye Hosteli ya Mtakatifu Martha iliyoko mjini Vatican, siku moja kabla ya uchaguzi wa Papa Mpya. Utaratibu wote utapangwa wakati wa mkutano wa Makardinali. Kikanisa cha Sistina ambacho kina utajiri mkubwa wa Sanaa kitafungwa rasmi kuanzia tarehe 28 Februari 2013 ili kutoa nafasi kwa ajili ya maandalizi ya mchakato wa uchaguzi wa Papa Mpya.







All the contents on this site are copyrighted ©.