2013-02-26 08:15:40

Yaani! Vatican hapatoshi!


Kardinali Agostino Vallini, Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma, anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kujitokeza kwa wingi katika Katekesi ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, inayotarajiwa kufanyika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, jumatano tarehe 27 Februari 2013, majira ya saa 4:30 asubuhi kwa saa za Ulaya. Hili litakuwa ni tukio la mwisho kwa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kuonekana hadharani kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Lengo la Jimbo kuu la Roma, ni kumshukuru kwa utume ambao amelitendea Jimbo la Roma kama Askofu wake katika kipindi cha miaka minane ya uongozi uliotukuka. Pale alipopata nafasi ya kutembelea Parokia, aliwalisha waamini wake kwa Neno la faraja anasema Kardinali Vallini. Amewawezesha waamini hao kuonja unyenyekevu, hekina na busara; amani na utulivu wa ndani kutoka kwa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita.

Huu ni wakati wa kusali kwa ajili pamoja na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, ili kumwombea kwa Kristo mchungaji mkuu wa Kanisa lake. Kutokana na idadi kubwa ya waamini na watu wenye mapenzi mema kutaka kushiriki katika tukio hili, Kardinali Vallini anasema kwamba, watu hawatalazimika kuwa na tiketi za kuingia kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, tiketi ni nguvu zako mwenyewe.

Kardinali Vallini anaendelea kuwahimiza waamini kusali kwa ajili ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, pamoja na kuendelea kuwaombea Makardinali watakaoshiriki katika mkutano wa kumchagua Papa mpya, ili waweze kutekeleza wajibu huu tete kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa kwa sasa na kwa siku zijazo!







All the contents on this site are copyrighted ©.