Wasomi wanachangamotishwa kutumia uwezo wao wa kiakili kuimarisha imani katika matendo!
Padre Francois Xavier Dumortier Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian, kilichoko
mjini Roma, anawaalika wanafunzi chuoni hapo kuungana na Baba Mtakatifu Benedikto
wa kumi na sita kwa ajili ya kuliombea Kanisa ili liweze kupata mchungaji mkuu atakayeliendeleza
baada ya Papa Benedikto wa kumi na sita, kung'atuka kutoka madarakani.
Kipindi
kama hiki kinasheheni majonzi na simanzi, lakini kwa njia ya sala na tafakari ya kina,
mwamini anaweza kutambua mpango wa Mungu katika hija ya maisha na utume wa Kanisa.
Kanisa linapenda kumshukuru Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kwa utume wake
kwa Kanisa katika kipindi cha miaka 8. Kama kielelezo cha shukrani kwa Baba Mtakatifu,
wanafunzi wote wa Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregoriani watashiriki katika Katekesi
ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, inayotarajiwa kufanyika kwenye Uwanja
wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, siku ya Jumatano, tarehe 27 Februari
2013.
Katika utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro ameonesha umuhimu wa
kumfuasa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu kwa njia ya huduma
makini inayobubujika na kufumbata imani. Ni kiongozi ambaye ameonesha ujasiri na ukomavu
wa kiimani; daima akajikita kutafuta ukweli kwa kutumia vyema vipaji na karama alizokirimiwa
na Mwenyezi Mungu. Ameonesha dira kwa wafuasi wa Kristo kwamba, wanapaswa kumependa
Mungu na jirani kama kielelezo cha imani tendaji. Ni kiongozi aliyekuwa na maneno
machache, lakini yaliyogusa na kuacha chapa ya kudumu.
Kwa hakika Baba Mtakatifu
Benedikto wa kumi na sita, amejitoa kimaso maso bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo
na Kanisa lake, akionesha fadhila ya unyenyekevu. Amekumbana na vikwazo na vizingiti
vingi, lakini ameendelea kusimama imara kutokana na imani kwa Kristo na ujasiri katika
ukweli. Alijitosa kulisafisha Kanisa la Kristo ili liendelee kuwa ni mchumba mwaminifu
wa Kristo. Kanisa linaendelea kufanya hija ya maisha na utume wake kwa kuifuata ile
Njia ya Msalaba, kwa kujikita katika fadhila ya unyenyekevu na upendo unaobubujika
kutoka kwa Kristo mwenyewe kwa ajili ya watu wake.
Urithi ambao Baba Mtakatifu
anapenda kuliachia Kanisa ni mapambano ya maisha ya kiroho, yanayomfungulia mwamini
mlango wa imani thabiti. Kama Jumuiya ya Wasomi, wanaalika na Baba Mtakatifu kuhakikisha
kuwa wanatumia kwa ukamilifu uwezo wao wa kufikiri na kutenda ili kuimarisha imani
pamoja na kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu
wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Huu ni ujumbe wa imani unakumbatia
Neno la Matumaini na maisha tele!