Wahamiaji na wageni watambuliwe, waheshimiwe na kuthaminiwa kama binadamu walioumbwa
kwa sura na mfano wa Mungu
Kardinali Antonio Maria VegliĆ², Rais wa Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji
kwa ajili ya wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi, Jumanne, tarehe 26 Februari, 2013
amekutana na kuzungumza na Kamati ya kiufundi ya Umoja wa Wafabiashara Wakristo nchini
Italia.
Anasema, Mama Kanisa anopoadhimisha Jubilee ya miaka hamsini ya Mtaguso
Mkuu wa Pili wa Vatican, anapenda kukazia umuhimu wa waamini pamoja na watu wote wenye
mapenzi mema kudumisha upendo na mshikamano wa dhati na wote wanaosukumizwa pembezoni
mwa Jamii kutokana na hali mbali mbali za maisha.
Kanisa ni Sakramenti ya
Umoja, kumbe, wahamiaji na wageni wajisikie kuwa ni sehemu ya Familia ya Mungu kwa
kuwaonjesha umoja, upendo na mshikamano wa dhati unaobubujika kutoka kwa Kristo mwenyewe.
Wote hawa wapokelewe kwa furaha, upendo na matumaini, ili kwa pamoja kujenga na kuimarisha
Familia ya binadamu.
Katika ulimwengu wa utandawazi, Mama Kanisa bado anaendelea
kuchangamotishwa kuhudumia kwa upendo, hasa wale wanaolazimika kuyakimbia makazi yao
kutokana na: maafa, njaa, vita, ukame na athari za mabadiliko ya tabianchi. Maendeleo
ya sayansi na teknolojia yamewawezesha watu wengi kuwa karibu zaidi, changamoto ya
kushirikiana kwa ajili ya kutafuta mafao ya wengi. Kuna mabadiliko makubwa ya kiuchumi
na kifedha yanayowafanya watu wengi kujisikia kuwa ni sehemu ya mchakato wa mabadiliko
haya katika Jamii, kiasi cha kuvutwa kutoka sehemu moja hadi nyingine, kila mtu akiwa
na sababu mbali mbali, wanakabiliana na vikwazo, lakini bado wanaendelea kusonga mbele
kwa imani na matumaini.
Badala ya kufunga mipaka, kuna haja ya kuimarisha
misingi ya haki za binadamu na kwamba, Kanisa katika Mafundisho yake Jamii linatambua
kwamba, kila mtu anayo haki ya kuhama kutoka sehemu moja hadi nyingine katika harakati
za kujitafutia maboresho ya maisha! Hii ni sehemu ya haki asilia. Wahamiaji wapewe
ulinzi na kuhakikishiwa usalama wa maisha yao. Wahamiaji kwa upande wao, watambua
urithi na tunu msingi za maisha ya kiroho na kijamii za wenyeji wao; wajitahidi kuheshimu
sheria za nchi pamoja na kutekeleza dhamana na majukumu yao ya kila siku.
Pale
inapowezekana Serikali za nchi husika ziboreshe hali na mazingira yatakayotoa hamasa
kwa wananchi kubaki katika maeneo yao kwani haki ya kwanza kwa kila mtu ni kubaki
katika nchi yake asilia. Athari za myumbo wa uchumi kimataifa, ukosefu wa mahitaji
msingi, fursa za ajira, maafa asilia, kinzani na migogoro ya kivita, kijamii, kisiasa
na kidini.
Haya ni kati ya matukio ambayo yameongeza wimbi la wahamiaji sehemu
mbali mbali za dunia. Hapa Mama Kanisa anachangamotishwa kujikita katika Uinjilishaji
Mpya, kwa kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu pamoja na matumizi
sahihi ya maliasili kwa ajili ya mafao ya wengi. Wahamiaji waheshimiwe kama binadamu
walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kamwe wasibaguliwe, kwani hata wao wanachangia
pia katika ustawi na maendeleo ya nchi husika.
Mshikamano anasema Kardinali
VegliĆ² una maanisha ile hali ya kuwajibika kwa kuwasaidia watu wanaoteseka katika
shida na mahangaiko mbali mbali. Wahamiaji waheshimiwe na kuthaminiwa kwani ni nguvu
kazi inayoweza kusaidia mchakato wa maendeleo katika nchi wahisani. Ni watu wenye
heshima na utu wao, wathaminiwe. Kanisa kama chombo cha wokovu, liwashirikishe imani,
matumaini na mapendo kwa kuwatambua kuwa ni sehemu ya Familia ya Mungu.