Tafadhali sitisheni biashara ya silaha ili kuokoa maisha ya wananchi wa Syria
Patriaki Gregory wa tatu Laham wa Kanisa Katoliki Madhehebu ya Kigriki nchini Syria
anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kusitisha biashara ya silaha na Syria kwani madhara
yake ni makubwa kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe inayoendelea nchini humo.
Watu wanaendelea kupoteza maisha yao na miundo mbinu kuharibiwa kwa sababu kuna kundi
la wafanyabiashara linalofaidika kutokana na biashara ya silaha nchini Syria.
Patriaki
Gregory wa tatu Laham anasema kwamba, umefika wakati kwa Jumuiya ya Kimataifa kuchukua
hatua za dhati ili kuanzisha mchakato wa majadiliano ya kisiasa ili haki, amani na
upatanisho viweze kutawala tena nchini Syria. Uchu wa faida kubwa kutokana na biashara
ya silaha isiifanye Jumuiya ya Kimataifa kushindwa kuona mateso na mahangaiko ya wananchi
wa Syria.
Anasema, Marekani na Russia ni wadau wakuu wa vita inayoendelea
nchini Syria, wakiamua, wanaweza kusaidia kupata suluhu ya kudumu. Kanisa kwa njia
ya sauti yake ya Kinabii pia linaalikwa kutekeleza wajibu wake ili amani ya kweli
iweze kupatikana tena nchini Syria.