2013-02-26 08:22:25

Bado Kristo anawatuma Wafuasi wake kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa ushuhuda wa maisha yao!


Hapo mwanzo, Neno alikuwako; naye alikuwa Mungu. Tangu mwanzo Neno alikuwa na Mungu. Alikuja katika nchi yake mwenyewe, nao walio wake hawakumpokea, wale waliomwamini aliwapa uwezo wa kuwa watoto wa Mungu. Hakuna mtu aliyemwona Mungu kamwe. Mwana wa pekee aliye sawa na Mungu ambaye ameungana na Baba ndiye aliyetujulisha habari za Mungu.

Wakati Yohane Mbatizaji alipokuwa anabatiza watu mtoni Yordani, wafuasi wawili wa Yohane Mbatizaji yaani Andrea na Nduguye Simoni Petro walimsikia akisema kuwa Yesu ndiye Mwana Kondoo wa Mungu wakaamua kuacha yote na kumfuata, kwani walitambua kwamba, wamekutana na Masiha, yaani Kristo.

Wafuasi wengi wa Yesu kama vile akina Andrea na Filipo walitoa ushuhuda wao juu ya utimilifu wa Unabii na Sheria kama ilivyobainishwa kwenye Maandiko Matakatifu. Itakumbukwa kwamba, Yesu kadiri ya Injili ya Luka, siku moja, Yesu alikuwa amesimama kando ya Ziwa Genesareti, akiwa amezungukwa na watu wengi, wakisikiliza Neno la Mungu, akaingia katika mashua ya moja iliyokuwa ya Simoni akamtaka aisogeze majini, mbali kidogo na ukingo wa ziwa. Akaketi, akafundisha umati wa watu akiwa ndani ya mashua.

Siku moja katika pita pita zake, Yesu alimwona mtoza ushuru kwa jina Lawi, akamwambia nifuate, akaacha yote akaamua kumfuata na kumwandalia Yesu karamu kubwa, akakaa pamoja na watoza ushuru, jambo ambalo lilipelekea Mafarisayo kuanza kunung’unika kwa kuwa alikua anakula na wadhambi pamoja na watoza ushuru. Lakini Yesu aliwajibu kwamba, wenye afya hawamhitaji tabibu bali wagonjwa ndio wenye shida kubwa, akawaambia kwamba, hakuja kuwaita wenye haki bali wadhambi ili watubu na kuongoka.

Wote hawa wameitwa kwa nyakati tofauti kutoka katika medani mbali mbali za maisha na utume wao, lakini wanatumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu. Tafakari hii ya Neno la Mungu iwasaidie waamini kuendelea kulitafakari Fumbo la Kanisa lililoanzishwa na Yesu, wakati huu, watu wengi wanapoendelea kumsindikiza Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kwa sala na sadaka yao kutokana na uamuzi wake wa kung’atuka kutoka madarakani.








All the contents on this site are copyrighted ©.