2013-02-26 08:17:39

Asante sana Baba Mtakatifu Benedikto XVI kwa unyenyekevu huu mkubwa!


Askofu mkuu Abune Berhaneyesus D. Souraphiel Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ethiopia na Eritrea, ameandika barua ya shukrani kwa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kutokana na uamuzi wake wa kung’atuka kutoka madarakani, alioufanya kwa utashi na uhuru kamili hapo tarehe 11 Fabruari 2013. Anasema, wameshtushwa sana na habari za kung’atuka kwa Baba Mtakatifu baada ya kulitumikia Kanisa Katoliki kwa miaka minane kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Maaskofu wanatambua kwamba, uamuzi huu umefikiwa baada ya kusali kwa muda mrefu, kufanya tafakari ya kina na kupembua kwa dhati dhamana na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro aliokuwa amekabidhiwa na Mama Kanisa, akaamua kung’atuka madarakani kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa. Anatambua kwamba, ulimwengu mamboleo una changamoto nyingi, unahitaji kiongozi mwenye nguvu za kiroho na kimwili na kasi zaidi katika utekelezaji wa majukumu ya Kanisa.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, amefanya maamuzi yenye ujasiri na Maaskofu wa Ethiopia na Eritrea kwa upande wao wanauheshimu na kuuthamini uamuzi huu na kwamba, wanaendelea kumwombea na kumpenda. Wanajiaminisha mikononi mwa Mwenyezi Mungu na kwa maongozi ya Roho Mtakatifu na kwa maombezi ya Bikira Maria, Mama wa Kanisa, kwa kuwaweka Makardinali wote watakaohudhuria mkutano wa kumchagua Papa mpya.








All the contents on this site are copyrighted ©.