Watawa wa ndani wanaalikwa kusali kwa ajili ya kuliombea Kanisa katika kipindi hiki
cha mpito!
Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican, amewaandikia barua wakuu wa Mashirika
ya Watawa wa ndani, kuwaomba kusali kwa ajili ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi
na sita pamoja na kuwaombea Makardinali watakaoshiriki kwenye mkutano wa kumchagua
Papa mpya, ili waweze kuongozwa na Roho Mtakatifu, wakijitahidi kusoma alama za nyakati
kwa Kanisa na Ulimwengu.
Baba Mtakatifu mwenyewe anaendelea kuwaomba waamini
na watu wenye mapenzi mema, kumsindikiza katika sala anapoachia madaraka mikononi
mwa Kristo mwenyewe, huku akiendelea kusubiri kwa imani na matumaini Papa mpya. Ni
mwaliko wa pekee kwa Mashirika ya Watawa wa ndani kusali kwa ajili ya Kanisa, kwani
sala za watawa zimelisindikiza Kanisa katika maisha na utume wake. Mkutano wa Makardinali
unategemea sala na masifu ya watawa wa ndani.
Changamoto ya kujiachilia mikononi
mwa Roho Mtakatifu kwa njia ya sala, ni mfano makini unaotolewa na Baba Mtakatifu
Benedikto wa kumi na sita, ambaye kwa miaka nane ameliongoza Kanisa na kwa sasa anang'atuka
kutoka madarakani, ili kupata muda mrefu zaidi wa kusali na kutafakari. Baba Mtakatifu
kwa upande wake, anawashukuru watawa na kuwahakikishia kwamba, anathamini ushuhuda
wao katika maisha na utume wa Kanisa.