Uamuzi wa Papa Benedikto XVI kung'atuka madarakani hauna budi kuheshimiwa!
Kung’atuka kwa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kutoka madarakani kumepokelewa
kwa hisia mbalimbali na mshangao mkubwa. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu
wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili yake na kwa ajili ya Kanisa, daima wakitumainia
neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Basi tumsindikize Baba Mtakatifu Benedikto
wa XVI kwa moyo wa shukrani na sala kwa tendo huru, ambalo amelitekeleza kutoka katika
dhamiri nyofu, mintarafu mwanga wa Injili. Ameamua jambo hili, kwa kutambua udhaifu
wake na mipaka inayotokana na “umri wake mkubwa” kiasi cha kumfanya kushindwa kutekeleza
utume wake kwa ukamilifu zaidi katika jamii inayokumbwa na mabadiliko makubwa na changamoto
mbalimbali. Ni maneno yaliyosikika kutoka kwa baadhi ya watu waliohojiwa na Radio
Vatican kwa nyakati mbali mbali. Wanasema “Tupokee uamuzi huu katika jicho la imani
kuwa ni fundisho la maisha ya kiroho linalofungua lango la Kanisa katika safari ya
maisha. Tunapofikiria uamuzi wake huo katika Mlango wa Imani tunaweza kutambua kwamba,
kung’atuka kwake ni kielelezo ch abusara na usomaji wa “alama za nyakati” na mwaliko
wa neema ya Mungu kwa ajili ya ujenzi wa udugu, umoja, upendo na mshikamano kwa kuweka
kando matamanio ya kidunia ili kushirikiana na Yesu Kristo katika ujenzi wa Ufalme
wa Mungu. Kristo ni mfano bora huduma kama alivyoonesha siku ile ya Alhamisi Kuu,
alipowaosha mitume wake miguu. Tuendelee kusali na kutafakari kwa tujikabidhi mikononi
mwa Roho Mtakatifu anayeendelea kutenda maajabu yake katika maisha yetu ya kila siku.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anasema, anapanda Mlimani ili kusali
na kutafakari zaidi na wala si kulikimbia Kanisa. Ni maneno yenye unyenyekevu wa hali
ya juu, ambayo baadhi ya vyombo vya habari vimeshindwa kuyazingatia kwa kutoa shutuma
zisizo na msingi kwamba, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anakimbia matatizo
na changamoto zinazolikabili Kanisa. Jumapili iliyopita maelfu ya watu kutoka sehemu
mbali mbali za dunia walifika mjini Vatican kumsindikiza Baba Mtakatifu Benedikto
wa kumi na sita kwa sala pamoja na kumuaga kwa majitoleo yake makuu kwa Kanisa la
Kristo kwa kipindi cha miaka minane. Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro ulikuwa
umefurika na kuwacha watu wengi wameshikwa na mshangao mkuu!