2013-02-25 07:58:21

"Napanda kwenda Mlimani ili kusali na kutafakari na wala si kulikimbia Kanisa"!


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Jumapili tarehe 24 Februari 2013, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, kwa mara ya mwisho kama Khalifa wa Mtakatifu Petro alitafakari kuhusu Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Kwaresima, inayomwonesha Yesu alipokuwa anasali Mlimani pamoja na wanafunzi wake watatu: Petro, Yakobo na Yohane, aligeuka sura. Hii ni hali inayoonesha Umungu wa Yesu Kristo.

Baba Mtakatifu anaendelea kueleza kwamba, kabla ya tukio hili, Yesu mwenyewe alikuwa amewaambia kuhusu mateso, kifo na ufufuko wake kutoka katika wafu. Tukio la Yesu kung’ara sura linaashiria utukufu wake, jambo ambalo pia lilijionesha wakati alipokuwa anabatizwa Mtoni Yordani, sauti kutoka mbinguni ikasema, “huyu ni mwanangu mpendwa wangu ambaye nimependezwa naye msikieni yeye”.

Uwepo wa Musa na Eliya ni kielelezo cha Sheria na Unabii katika Agano la Kale na historia ya Agano kati ya Mungu na mwanadamu inapata utimilifu wake kwa njia ya Yesu Kristo anayemkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na kumwelekeza katika nchi ya ahadi si kama ile iliyojaa maziwa na asali wakati wa Musa, bali Kristo anawapeleka mbinguni.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anasema kwamba, tukio hili lilimwacha Mtume Petro akiwa ameshikwa na bumbuwazi, kiasi hata cha kukosa maneno ya kuzungumza na hatimaye anaishia kusema, "Bwana inapendeza sisi kukaa hapa” Ni maneno yanayoonesha jinsi ambavyo ni vigumu kuweza kuweza kukumbatia “Fumbo hili”. Mtakatifu Agostino, Askofu na Mwalim wa Kanisa, anafafanua kwamba, hapa Mlimani, Mtume Petro alikuwa amempata Yesu kama chakula chake cha kiroho, kiasi kwamba, hakuona tena sababu za msingi kushuka kutoka mlimani na kuanza kuteseka tena, wakati alikwisha onja utimilifu wa upendo wa Mungu.

Baba Mtakatifu anasema, sehemu hii ya Injili ina utajiri mkubwa katika maisha ya waamini, kwanza kabisa inakazia umuhimu wa maisha ya sala inayomwilishwa katika matendo. Kipindi cha Kwaresima, iwe ni fursa kwa kila mwamini kutoa kipaumbele cha kwanza kwa sala binafsi na ile ya Kijumuiya, jambo muhimu katika maisha ya kiroho. Kwa njia ya sala, si kwamba, mwamini anajitenga na ulimwengu, kama Mtume Petro alivyotamani pale Mlimani Tabor.

Mwamini hana budi kuhakikisha kwamba, daima anafanya hija ya kupanda mlimani ili kuweza kukutana na Mwenyezi Mungu katika hija ya maisha yake na baadaye kushuka chini akiwa amesheheni upendo na nguvu alizojichotea kutoka kwa Mungu, ili aweze kuwatumikia jirani zake mintarafu upendo wa Mungu.

Baba Mtakatifu anasema, kwa namna ya pekee anasikia kwamba, sehemu hii ya Injili inamgusa kwa namna ya pekee wakati huu wa maisha yake, kwani Mwenyezi Mungu anamwita kupanda mlimani, ili kusali na kutafakari zaidi. Hii haina maana kwamba, analikimbia Kanisa, bali ni changamoto ya kulitumikia Kanisa kwa moyo na upendo mkuu zaidi, kama alivyojitahidi kufanya hadi sasa, lakini kwa wakati huu anapaswa kutekeleza utume huu kadiri ya umri na nguvu alizo nazo. Anawaalika waamini kumwomba Bikira Maria aweze kuwasaidia kumfuasa Kristo daima kwa njia ya sala na matendo ya huruma.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, alihitimisha tafakari yake ya mwisho kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, akiwashukuru waamini, mahujaji na watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, waliofurika kwenye viunga vya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican ili kuweza kumshukuru na kumuaga Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kutokana na uamuzi wake wa kung’atuka kutoka madarakani kwa utashi na uhuru kamili.

Kwa hakika, hili ni tukio ambalo limewagusa wengi na litaendelea kubaki kama kumbu kumbu endelevu katika miyo ya watu wengi kutokana na ujasiri na unyenyekevu uliooneshwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita. Amewashukuru na kuwaambia wote kwamba, wataendelea kuwa pamoja kwa njia ya sala.








All the contents on this site are copyrighted ©.