Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, wakati anatangaza kung’atuka kutoka madarakani
aliwaambia waamini kwamba, analiaminisha Kanisa kwa mchungaji mkuu Yesu Kristo. Alisema
kwamba, ana mang’amuzi na uhakika kwamba, Kanisa ni la Kristo atalipatia mchungaji
mkuu kwa wakati wake. Ni maneno yanayowakumbusha waamini utambulisho wa Kanisa
kwamba, si kama taasisi nyingine nyingi zinazofahamika, bali hili ni Kanisa lililoanzishwa
na Yesu Kristo mwenyewe, kama Jumuiya ya waamini ambayo imeendelea kufanya hija yake
katika historia na sehemu mbali mbali za dunia, likitolea ushuhuda wa uwepo wa Mungu
kati ya watu wake. Hii ni sehemu ya kazi ya ukombozi iliyotekelezwa kuanzia kwa
akina Ibrahim Baba wa Imani, Watu wa Agano la Kale na kupata utimilifu wake katika
maisha ya Yesu wa Nazareti; Neno na Tukio muhimu linaonesha ufunuo wa Mungu, unaopania
kuenzi utu, heshima na utimilifu wa maisha ya mwanadamu. Hii ni tafakari kutoka kwa
Padre Francesco Rossi de Gasperis, mtaalam wa Maandiko Matakatifu anayependa kuwashirikisha
waamini na watu wenye mapenzi mema ufahamu wa kina kuhusu Fumbo la Mwili wa Kristo,
yaani Kanisa na umuhimu wa utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kuna tofauti ya
kubwa kati ya dini ya Kikristo na dini nyingine duniani. Kuna baadhi ya dini zinajitahidi
kujenga uhusiano na Mwenyezi Mungu. Hizi ni jitihada za tafiti kuhusiana na Mungu
na matokeo yake zinapata vielelezo, ibada. Lugha na sala kutokana na mahali pamoja
na mazingira husika. Ukristo pia umepia hatua kama hii, lakini tofauti ni kwamba,
hapa Mwenyezi Mungu ndiye anayeanza mchakato wa kumtafuta Mwanadamu, akimwonesha imani
thabiti yenye mwendelezo kutoka kwa Ibrahim Baba wa Imani hadi kwa Yesu, akitoa mwaliko
wa kuweza kujiunga naye ili aweze kumwinua. Ukristo ni dini ya imani inayojikita
katika Neno la Mwingiliano ambao umewezeshwa kwa nguvu ya Roho Mtakatifu anayeimarisha
hatua zote zinazochukuliwa na binadamu katika hija ya historia ya maisha yake, tangu
pale katika kazi ya uumbaji hadi nyakati za mwisho. Yesu wa Nazareti ni Mwana wa Mungu
aliyetwaa mwili, aliyeteswa, akafa na kufufuka. Hili ndilo Fumbo la Pasaka linalowaunganisha
waamini katika hija ya kuyaendelea maisha ya uzima wa milele. Yesu anaendelea
kulijenga na kuimarisha Kanisa lake, hadi pale litakaposhiriki utukufu wa Kristo katika
Yerusalemu ya mbinguni. Mwenyezi Mungu aliyefanya maagano na watu mbali mbali katika
Maandiko Matakatifu ndiye anayeendelea kulitegemeza Kanisa lake kwa njia ya Khalifa
wa Mtakatifu Petro, Mwamba hai ambalo unashikilia Kanisa la Kristo. Baba Mtakatifu
Benedikto wa kumi na sita katika kipindi hiki cha Kwaresima sanjari na Maadhimisho
ya Mwaka wa Imani, anawaalika waamini kuchuchumilia toba na wongofu wa ndani, kwa
kutoa nafasi kwa Mwenyezi Mungu ili kuweza kukabiliana na changamoto za maisha ya
kila siku kwa imani na matumaini. Ni mwaliko wa kung’oa ndago za ubinafsi kwa kujishikamanisha
na upendo kwa Mungu na jirani. Waamini wakumbatie Fumbo la Msalaba na kamwe wasing’ang’anie
madaraka na mali za dunia bali kipaumbele kiwe ni kwa ajili ya kuendeleza kazi ya
ukombozi iliyoanzishwa na Mwenyezi Mungu mwenyewe. Kutubu na kuongoka anasema Baba
Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, maana yake si kujitafuta mwenyewe wala nafasi
katika Jamii, bali kuhakikisha kwamba, kila siku ya maisha ukweli, imani na mapendo
kwa Mungu yanajidhihirisha. Wakati huu waamini wanaalikwa kufarijika na Neno la Mungu
pamoja na neema zinazobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, zinazowapatia
nguvu ya kumwita Mungu, Abba, yaani Baba.