2013-02-25 09:53:39

Familia ya Mungu nchini Uingereza inamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Benedikto XVI kwa maisha na utume wake!


Askofu mkuu Vincent Nichols, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza, Jumapili tarehe 24 Februari 2013 aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu iliyohudhuriwa na waamini, viongozi wa Kanisa na wawakilishi wa taasisi mbali mbali za Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza kwa nia ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, baada ya kuamua kwa utashi na uhuru kamili kung'atuka kutoka madarakani.

Askofu mkuu Nichols anasema, hili ni tendo la ujasiri na unyenyekevu mkubwa na kwamba, ni changamoto kwa waamini kuendelea kujenga uhusiano wa dhati na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Sala na Tafakari ya kina ya Neno la Mungu; daima wakijitahidi kujenga na kuimarisha umoja, upendo na mshikamano wa Kanisa.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, amekuwa kwa hakika kiongozi ambaye alijitoa kimaso maso katika utume na maisha yake, ili Kanisa la Kristo liweze kukua na kushamiri, huku likitoa huduma kwa Familia ya Mungu, kwa njia ya Utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu na Matendo ya huruma, haki, amani na upatanisho kwa wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Ni kiongozi aliyekazia Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu kama njia ya kuzungumza na Kristo kutoka katika undani wa maisha, Vijana wa Uingereza walionja ushuhuda huu wakati wa hija yake ya kichungaji nchini Uingereza, walipokaa kwa takribani dakika kumi na tano kwa kimya kikuu, wakitafakari kuhusu upendo wa Kristo unaojionesha kwa namna ya pekee katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu.

Askofu mkuu Nichols anasema, Baba Mtakatifu si mtu aliyekuwa anatafuta makuu, bali alitaka Kanisa la Kristo lipendwe, liheshimiwe na kuthaminiwa. Alitamani kuwaona waamini wakikumbatia imani na akili kama kipimo makini cha kanuni maadili, kwani imani si tatizo linalopaswa kupatiwa ufumbuzi, bali hazina ambayo haina budi kuvumbuliwa.

Baba Mtakatifu anajiandaa kung'atuka kutoka madarakani, ili aweze kupata muda mrefu zaidi katika sala, tafakari pengine na kuandika vitabu. Kanisa linatambua na kuthamini mchango wake; alithamini hata mchango wa wale ambao, kimsingi hawakukubaliana na mawazo yake. Ni kiongozi ambaye kwa hakika ameonesha fadhila ya matumaini inayobubujika kutoka kwa Kristo mwenye uwezo wa kufanya mabadiliko makubwa katika maisha na utume wa Kanisa lake.

Askofu mkuu Nichols anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kusali ili kumwomba Roho Mtakatifu aliwezeshe Kanisa kupata Kiongozi mkuu na Makardinali watakaoshiriki katika mkutano wa kumchagua Papa mwingine waweze kutekeleza wajibu wao kikamilifu.







All the contents on this site are copyrighted ©.