Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika, IMBISA, hivi karibuni
limekutana na kufanya mazungumzo na Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, kama ambavyo pia
waliwahi kuzungumza naye kabla ya mkutano wao mkuu uliofanyika kunako mwaka 2001 na
mwaka 2004.
Maaskofu wa IMBISA wanapongeza hali ya mshikamano na umoja wa
kitaifa inayoendelea kujionesha kama kielelezo cha matumaini mapya katika mchakato
wa kufufua uchumi na kujikita katika maendeleo ya wananchi wa Zimbabwe. Maaskofu wanasema,
Kanisa linaunga mkono demokrasia ya kweli, umuhimu wa kulinda na kuheshimu Katiba
ya nchi ambayo ni sheria mama; haki za binadamu na umuhimu wa kila raia kutekeleza
wajibu na dhamana yake ndani ya Jamii husika.
Kanisa linapania kusimama kidete
kutetea: haki, mafao ya wengi, uchaguzi huru na wa haki pamoja na kushirikiana kwa
karibu zaidi na tume ya uchaguzi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi. Maaskofu
wa IMBISA wanaendelea kuonesha mshikamano wao na wananchi, katika zile nchi ambazo
zinajiandaa kwa ajili ya kufanya uchaguzi mkuu kwa mwaka 2013.
Wanawaalika
waamini, wananchi na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, chaguzi zinazingatia:
amani, uhuru, ukweli na uwazi. Kusiwepo na madhulumu ya kisiasa bali kila Chama cha
kisiasa kizingatie na kuheshimu Katiba ya nchi ambayo inatakiwa kupigiwa kura ya maoni
na wananchi wa Zimbabwe.
Serikali ya Umoja wa Kitaifa ihakikishe kwamba, hata
wapinzani wanapata nafasi ya kutumia vyombo vya mawasiliano ya Jamii vinavyomilikiwa
na kuendeshwa na Serikali.