2013-02-22 09:18:08

Upatanisho na haki ni misingi mikuu ya amani katika Jamii!


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika Waraka wake wa kichungaji, Dhamana ya Afrika, Africae Munus anabainisha kwamba, upatanisho na haki ndiyo misingi mikuu ya amani ambayo kimsingi ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, lakini inamshikirisha mwanadamu katika maamuzi na vipaumbele vyake.
Upatanisho na haki ni mambo yanyofumbatwa katika ukweli na upendo. Hii ni changamoto kwa Familia ya binadamu kujipatanisha na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani. Wakristo wanaendelea kuchangamotishwa kuwa kweli ni mfano wa kuigwa katika medani ya haki na upendo.
Askofu Mkuu Josephat Lebulu, wa Jimbo kuu la Arusha, katika Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuombea amani nchini Tanzania iliyofanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu, hapo tarehe 20 Februari 2013 amesema, Wakristo wanao uwezo wa kulipiza kisasi dhidi ya mauaji ya viongozi wao yanayofanywa na watu wasiopenda haki na amani, wanaotumiwa na watu ndani na nje ya Tanzania, lakini Kristo, anawataka wasilipize kisasi ili kutompatia shetani ushindi.
“Sisi siyo wapumbavu na kwamba hatuwezi kufanya chochote…tunavutwa tu na huruma ya Mwenyezi Mungu tukae kimya, lakini hakuna mwanadamu yeyote anayeweza kuvumilia hili. Katika mazingira halisi ya kibinadamu, hakuna hata mmoja ambaye atafurahia mauaji haya isipokuwa shetani na mawakala wake,” alisema.
Askofu mkuu Lebulu anawaalika Wakristo na waumini wa dini nyingine wenye mapenzi mema, wasitawaliwe na hasira, chuki wala mioyo ya kulipa kisasi kwa sababu Yesu Kristo amewataka wasifanye hivyo, ingawa uwezo wa kufanya hivyo wanao na haki ingekuwa upande wao. Alisema hayo katika mahubiri yake ya Misa ya Wafu ya kumwombea marehemu Padri Mushi.

Askofu Mkuu Lebulu, alisema: “Tusilipe kisasi, bali tushinde kwa yaliyo mema.” “Kama Mungu yupo nasi na yupo upande wetu, hata kama kwa mabavu na bunduki, hakuna wa kututenganisha na upendo wa Kristo. Je, ni dhiki, njaa, uchi, hatari au upanga,” alihoji na kuongeza: “Lakini haya yote tunayashinda kwa Jina la Yesu na yeye anatupenda na hakuna chochote kitakachotutenga na upendo wa Kristo.” Ibada hii ilihudhuriwa na umati mkubwa wa waamini na wapenda amani Jimbo kuu la Arusha.
Akizungumzia mauaji ya viongozi wa Kikristo nchini Tanzania alisema, wanaamini ukweli wa mambo hayo utajulikana maana hakuna kinachotendeka kwa siri ambacho hudumu hivyo hivyo bila kujulikana. Askofu Mkuu Lebulu, alisema Watanzania wanalia kama watoto yatima kwa kukosa Baba au Wazazi na akaelezea kushangazwa kwake kuhusu kauli za vitisho, matusi na kuleta hofu zilizokuwa zikisambazwa na baadhi ya watu kwa njia za CD, DVD, kanda na ujumbe wa simu, huku vyombo vya usalama vikitazama tu, halafu baadaye wanalalamika maadili yameshuka.

“Unashangaa vyombo vya usalama vinaangalia tu, zipo kanda nyingi za matusi na vitisho dhidi ya waamini wa dini nyingine…vipo wapi vyombo vya usalama kama wengine wanauawa namna hii. Mungu awaguse mioyo yao na wabadilike na kumgeukia Mungu “Mambo hayo watu wa usalama wamezembea, tangu awali kulikuwapo na viashiria vingi sana vya kuwapo hofu ya mauaji, lakini kwa nini hawashughulikiwi, kisheria?” alihoji na kuongeza, “pengine hapa kuna siri imejificha.”

Alilaani pia mauaji ya Mchungaji Mathayo Kachira (45), wa Kanisa la Pentekoste la Assemblies of God, mkoani Geita, uchomaji moto wa makanisa na tukio la kumwagiwa tindikali kwa Sheikh huko Zanzibar, kunakofanywa na baadhi ya watu kwa malengo wanayoyajua wao wenyewe na akasema vitendo hivyo havisaidii kuleta amani, upendo na mshikamano wa kitaifa. Kuna haja kwa watanzania kuanza mchakato wa kujenga misingi ya haki, amani na upatanisho wa kitaifa, kwa kuzingatia kwanza kabisa mafao ya wengi pamoja na kujitahidi kujenga mfumo wa haki jamii.









All the contents on this site are copyrighted ©.