Maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013
Vijana Wakatoliki kutoka Majimbo mbali mbali nchini China wameanza maandalizi ya kiroho
yatakayowawezesha kushiriki kikamilifu katika Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani,
itakayofanyika mjini Rio de Janeiro nchini Brazil, kuanzia tarehe 23 hadi tarehe 28
Julai 2013. Maandalizi yanayoendelea kwa sasa sehemu mbali mbali za dunia ni kuwawezesha
vijana kujisikia kuwa kweli ni Wamissionari wanaotumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu
kwa Watu wa Mataifa, kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao adili na manyofu. Vijana
wanapaswa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kutambua kwamba,
kama Wafuasi wa Kristo wanatumwa kutangaza Kweli za Kiinjili. Jumla ya vijana thelathini
kutoka Jimbo kuu la Hong Kong Kao Po wanatarajiwa kuwa ni sehemu ya wajumbe watakaoshiriki
katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani yanayokwenda sanjari na Maadhimisho ya
Mwaka wa Imani. Vijana watakaobaki Jimboni humo, wataungana na wenzao kiroho kwa shughuli
mbali mbali zitakazopangwa na Idara ya Utume kwa Vijana. Kanisa linataka kuwajengea
vijana uwezo wa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa, wakitambua
kwamba, wao ni jeuri na tumaini la Kanisa kwa sasa na kwa siku zijazo. Pale vijana
hawa wanapojisikia kuwa na wito wa maisha ya Kipadre na Kitawa, wasisite kujitokeza
mbele, tayari kuanza hija ya majiundo yatakayowawezesha siku moja kuwa ni wahudumu
wa Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na Matendo ya Huruma, yanayodhihirisha kwa
namna ya pekee, Imani tendaji.