2013-02-22 11:42:29

Bado kuna mamillioni ya watu wanakabiliwa na baa la njaa nchini Mali


Shirika la Mpango wa Chakula Duniani linasema, kuna zaidi ya watu millioni kumi ambao wanakabiliwa na baa la njaa kwenye Ukanda wa Sahel. Hali hii imesababishwa na kipindi cha miaka saba ya ukame uliojitokeza kwa kiasi kikubwa kunako mwaka 2005.

Idadi ya watu wanaopoteza maisha yao kutokana na baa la njaa katika Ukanda wa Sahel inapungua kwa kiasi kikubwa, lakini bado baa la njaa linaendelea kutishia maisha ya mamillioni ya watu. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujiwekea mikakati ya kupambana na baa la njaa kwa sasa na kwa siku za usoni. Hayo yamebainishwa hivi karibuni na Ertharin Cousin, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani.

Hali ya chakula nchini Somalia inaendelea kuboreka kidogo, lakini kuna haja ya kujipanga zaidi kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa Mali, ili msaada wa chakula uweze kuwafikia watu wengi zaidi. Ili kufikia lengo hili kuna haja pia kwa majeshi yanayopigana nchini Mali kutoa ruhusa kwa Mashirika ya Misaada Kimataifa kupeleka huduma kwa wahitaji nchini humo.







All the contents on this site are copyrighted ©.