2013-02-21 08:59:09

"Watanzania msikubali kushindwa na uwovu!


Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Jumatano tarehe 20 Februari 2013, ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumwombea marehemu Padre Evaristi Mushi aliyefariki dunia hivi karibuni kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana. Ibada hii imehudhuriwa na viongozi wa kidini, serikali, vyama vya siasa na watu wenye mapenzi mema.

Askofu mkuu Francisco Montecillo Padilla, Balozi wa Vatican nchini Tanzania, alisoma salam za rambi rambi kutoka kwa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, akieleza kushtushwa sana na mauaji ya Padre Evaristi Mushi. Baba Mtakatifu anaendelea kuwatia shime Wakristo nchini Tanzania kusonga mbele kwa imani, matumaini na mapendo na kamwe wasikatishwe tamaa kwa madhulumu na mauaji yanayotokea. Waendelee na utume wao kwa kujifunza kusamehe na kuwapenda adui, kama alivyofanya Yesu pale Msalabani.

Kifo cha Padre Evaristi Mushi si mapenzi ya Mungu, bali ni watu wameamua kukatisha maisha yake, kiasi kwamba wamemnyima nafasi ya kutekeleza utume wake kama Padre. Hii ni sehemu ya majaribu ya imani, Askofu mkuu Padilla anaamini kwamba, Yesu Kristo atawatia nguvu na ari ya kuweza kutekeleza utume wao kwa matumaini makubwa zaidi.

Askofu Tarsisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mahubiri yake, aliwataka waamini kusamehe na kusahau ili waendelee kuwa ni wajenzi wa misingi ya haki, amani, upendo na upatanisho wa kitaifa. Ni kujifunza kusamehe hata pale wanapokabiliwa na mauaji kama yalivyotokea kwa Padre Evaristi Mushi.

Askofu Augustino Shao wa Jimbo Katoliki Zanzibar katika salam zake amewataka watanzania kutokubali kukumbatia maovu kwa kutoa visingizio kuwa ni "mapenzi ya Mungu". Haya ni mauaji yaliyofanywa na watu wenye nia mbaya kwa Kanisa na maendeleo endelevu ya imani yao. Aliwashukuru wote waliofika Jimboni humo ili kumsindikiza Marehemu Padre Evaristi Mushi katika usingizi wa amani, akiwa na tumaini la uzima wa milele.

Viongozi mbali mbali wa kidini Zanzibar wanaelezea kwamba, hawana tena imani na Jeshi la Polisi kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake wa kulinda raia na mali zao mintarafu Katiba na sheria za nchi. Uhuru wa kuabudu na zawadi ya maisha ni mihimili muhimu sana katika kulinda na kutetea haki msingi za binadamu.

Waamini wa Kanisa Katoliki nchini Tanzania walitumia siku ya Jumatano kwa ajili ya kusali ili kuombea amani na utulivu wakati huu Tanzania inapokabiliwa na hali tete ya dalili za machafuko ya kidini. Katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoendeshwa na Askofu msaidizi Eusebius Nzigilwa wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yosefu, Padre Ambrose Mkenda aliyenusurika na kifo alipata nafasi ya kuwapungua mkono waamini waliokuwa wamefurika Kanisani hapo.

Marehemu Padre Evaristi Mushi alizaliwa tarehe 15 Juni 1957, Jimboni Moshi na amefariki dunia hapo tarehe 17 Februari 2013 kwa kupigwa risasi na kuzikwa kwenye Makaburi ya Kanisa Katoliki yaliyoko eneo la Kitope, Zanzibar. RIP.







All the contents on this site are copyrighted ©.