Umoja wa Mataifa wazindua "Mwaka wa Kimataifa wa zao la "Quinoa" katika mchakato wa
kupambana na baa la njaa, utapiamlo na umaskini duniani
Josè Graziano da Silva, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa
Mataifa, FAO, katika uzinduzi wa Mwaka wa Kimataifa wa Mazao ya Nafaka, kwenye Makao
Makuu ya Umoja wa Mataifa, anasema, mazao ya nafaka yana mchango mkubwa katika mapambano
dhidi ya baa la njaa, utapiamlo na umaskini duniani sanjari na kuhakikisha kwamba,
kuna uhakika wa usalama wa chakula duniani.
Sherehe za uzinduzi huu zimehudhuriwa
pia na Bwana Ban Ki-Moon, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa pamoja na viongozi wengine
wa kisiasa. Anasema, zao la nafaka linalojulikana kama "Quinoa" lina utajiri mkubwa
wa virutubisho vinavyohitajika katika mwili wa binadamu na kwamba, ni zao linaweza
kustahimili ukame, hali mbali mbali za hewa na udongo na hivyo kusaidia katika mchakato
wa mapambano ya baa la njaa na utapiamlo duniani.
Zao hili linaweza kuwa ni
tegemeo kubwa la chakula bora kwa idadi ya watu inayozidi kuongezeka duniani, huku
ikikabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na wasi wasi kuhusu hali
ya usalama wa chakula duniani. Zao hili linaweza kuwa ni chakula mbadala kwa siku
za usoni. Ni zao ambalo linaendelea kufanyiwa majaribio nchini Kenya na Mali na kwamba,
majaribio ya awali yanaonesha kwamba, linaweza kustawi sehemu mbali mbali za dunia.
Katibu
mkuu wa Umoja wa Mataifa anasema, kati ya Malengo ya Maendeleo ya Millenia ni kuhakikisha
kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inapunguza kwa kiasi kikubwa baa la njaa duniani; kwa
kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula pamoja na kupambana na umaskini.