2013-02-21 11:08:54

Mawazo ya Baba Mtakatifu Benedikto XVI kuhusu: binadamu na utamaduni kuanzia mwaka 1972 hadi mwaka 2005 yamekusanywa katika kitabu kimoja


Mada kumi na nne zilizoandikwa na Kardinali Joseph Ratzinger kuanzia mwaka 1972 hadi mwaka 2005 kabla ya kuteuliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, zimekusanywa na kuchapishwa katika kitabu kimoja kinachojulikana kama "Joseph Ratzinger in Communio: Anthrolopology and culture", na kuhaririwa na David L. Schindler na wenzake.

Baadhi ya mada zinazojadiliwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita ni: ubinadamu, dhana ya uzazi na kazi ya uumbaji; Yesu Kristo kwa nyakati hizi; maana ya Siku ya Bwana; Fadhila ya Matumaini; teknolojia ya usalama inayojadiliwa kwa jicho la kimaadili pamoja na dhana ya Mungu mintarafu Mafundisho ya Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili.

Kitabu cha kwanza chenye mkusanyo wa mada zilizoandikwa na Kardinali Joseph Ratzinger wakati huo kuhusu "Umoja wa Kanisa" kilichapishwa kunako mwaka 2010. Lengo ni kuona mchango wa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita katika uelewa wa: Kanisa, binadamu na mabadiliko ya mwenendo wa taalimungu. Itakumbukwa kwamba, Jarida la "Communio" lilianzishwa kunako mwaka 1972 na wanataalimungu mahiri kama akina Hans Urs von Balthasar, Henri de Lubac, Jean Luc Marion na Joseph Ratzinger mwenyewe.







All the contents on this site are copyrighted ©.