Caritas Sahel na mikakati ya kuwajengea wadau uwezo wa kupambana na majanga!
Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Ukanda wa Sahel, Caritas linaendelea na mkutano
wake uliofunguliwa hapo tarehe 19 na unatarajiwa kuhitimishwa tarehe 23 Februari 2013.
Wajumbe wanajadili pamoja na mambo mengine hali ya kisiasa, kijamii na baa la njaa
katika Ukanda wa Sahel ili kuweza kujipanga vyema zaidi kuokoa maisha ya watu. Mkutano
unawashirikisha wajumbe wa Caritas kutoka: Burkina Faso, Mali, Niger na Senegal, nchi
ambazo tangu mwaka 2007 zimeandaa Jukwaa la Mikakati ya Caritas Ukanda wa Sahel.
Wajumbe
wanataka kuimarisha mawasiliano katika kukabiliana na hali mazingira magumu kwa kujenga
uwezo kwa Mashirika ya Caritas katika nchi husika, ili kushiriki kikamilifu katika
kuwahudumia wahanga wa machafuko ya kivita nchini Mali. Hadi sasa takwimu zinaonesha
kwamba, kuna jumla ya watu zaidi ya 300,000 ambao wamekimbia kutoka Mali na wanapata
hifadhi katika mipaka ya nchi jirani.