Muasisi wa Mpango wa uzazi kwa njia ya asili afariki dunia!
Dr. Evelyn Livingston Billings, muasisi wa mpango wa uzazi kwa njia ya asili, amefariki
dunia Jumamosi, tarehe 16 Februari 2013 akiwa na umri wa miaka 95. Dr Evelyn pamoja
na mume wake Dr. John Billings kwa pamoja walianza mpango wa uzazi kwa njia ya asili,
mpango ambao kwa wengi unajulikana kama "Billings".
Baada ya kufanya utafiti
wa kina kuhusiana na zoezi la unyonyeshaji kwa wazazi pamoja na kuchunguza hali ya
wanawake waliokuwa wanakaribia kipindi cha ukame, alifanikiwa kutoa mchango mkubwa
katika maisha ya ndoa na familia. Kwa miaka hamsini, Madaktari hawa wametembelea sehemu
mbali mbali za dunia ili kufundisha mpango wa uzazi kwa njia ya asili, mpango ambao
unaungwa mkono na Mafundisho Jamii ya Kanisa kwa kuenzi Injili ya Uhai, dhidi ya Utamaduni
wa kifo unaokumbatia sera za utoaji na vizuia mimba.
Kwa mara ya kwanza kitabu
kuhusu mpango wa uzazi kwa njia ya asili kilitolewa kunako mwaka 1980, kikachapishwa
kwa mara 16 katika lugha 22 za Kimataifa. Kwa mara ya mwisho kitabu hiki kimechapishwa
kunako mwaka 2011. Dr. Evelyn aliwahi kuwa Mjumbe wa Taasisi ya Kipapa ya Maisha.
Katika uhai wake alibahatika kupata watoto 9 na mmoja amekwisha fariki dunia. Ameacha
wajukuu 39. Mume wake, Dr. John Billings alifariki dunia kunako mwaka 2007.