Ibueni mikakati kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watu wenu!
Waziri Mkuu Mizengo Pinda wa Tanzania, ameuagiza mkoa mpya wa Simiyu kuibua miradi
mikubwa ya kiuchumi ya kilimo na viwanda ili kuharakisha maendeleo ya mkoa huo badala
ya kukazania kujenga majengo makubwa ya kisasa ya ofisi. Alikuwa akifungua kikao
cha kwanza cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kwenye ukumbi wa KKKT mjini Bariadi,
makao makuu ya Simiyu, Jumanne Feb. 19, 2013) pamoja na kuhutubia mkutano wa hadhara
uwanja wa Saba Saba na na kupokea ripoti ya mkoa, Jumatatu, tarehe 18 Februari 2013.
Simiyu,
ambayo pamoja na Geita, Katavi na Njombe ni Mikoa mipya iliyoanzishwa hivi karibuni,
inazalisha karibu asilimia 50 ya pamba yote nchini na ina ng’ombe wapatao Milioni
1.5 na watu wanaokadiriwa kufikia milioni 1.6. “Mnaweza kuzitumia fursa na rasilimali
hizi kuleta maendeleo. Lakini mkikazania kujenga majengo makubwa na ya kisasa ya Ofisi
ya Mkuu wa Mkoa na Wakuu wa Wilaya, mtagundua baadaye kuwa hamjawasaidia hata kidogo
wananchi wenu,” alisema.
Mkoa wa Simiyu ulianzishwa rasmi Machi, 2012 na pamoja
na ile mingine mipya mitatu, inafanya idadi ya mikoa yote ya Tanzania Bara kuwa 25.
Waziri Mkuu Pinda alisema Serikali huanzisha maeneo mapya ya utawala kusogeza uongozi
na utawala karibu na wananchi ili usimamiaji wa shughuli za maendeleo na huduma za
jamii uwe na tija zaidi.
Pinda aliwaambia Wajumbe wa kikao hicho kuwa mkoa
huo unaweza ukafanya sherehe za uzinduzi wake, lakini siyo kwa mbwembwe, ila utumie
sherehe hizo kuwakaribisha wawekezaji binafsi waone fursa za kuwekeza katika mkoa
huo.
Akitoa shukrani kwa niaba ya Kamati ya Ushauri ya Mkoa, Mtemi Andrew Chenge,
ambaye pia ni Mbunge wa Bariadi Magharibi, alisema maelekezo yote yaliyotolewa na
Waziri Mkuu kwa Kamati hiyo ya maendeleo yatashughulikiwa kwa uzito wake wote. Baadaye
alasiri, Waziri Mkuu alitembelea mnada wa ng’ombe na mnada wa vitu vya kawaida vya
matumizi ya kila siku mjini Bariadi kujionea mwenyewe uendeshaji wa shughuli hizo
na kuzungumza na wafanyabiashara, wachuuzi na wanunuzi.