Jeshi la Polisi Mkoani Mbeya, Tanzania limetoa wito kwa taasisi binafsi na jamii kushirikiana
na Jeshi hilo katika kuhakikisha wakazi wa Mbeya wanaishi kwa hali ya utulivu na amani
kama wanavyoonesha ushirikianao tume ya haki na amani Jimbo Katoliki la Mbeya na hatimaye
kutunukiwa hati ya ushirikiano mwema.
Akikabidhi vyeti kwa wadau mbalimbali
wa ulinzi na usalama mkoani Mbeya Kamanda wa Polisi mkoani wa Mbeya, Diwani Athumani
amesema jukumu la ulinzi na usalama ni la kila mtu, Serikali na sekta binafsi hivyo
kila mmoja kwa nafasi yake anapaswa kuhakikisha mali na maisha ya kila mtanzania yanakuwa
salama pamoja na mali zao.
Kamanda Diwani amesema Tume ya Haki na Amani, Jimbo
Katoliki Mbeya ni miongoni mwa wadau muhimu wa ulinzi na usalama mkoani Mbeya katika
kipindi cha mwaka 2012 na hivyo ametoa rai kuendelea kuwa wadau muhimu katika eneo
hilo nyeti kwa mwaka 2013 hili kuendelea kulinda misingi hiyo iliyoachwa na hayati
Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kamabarage Nyerere.
Akipokea hati hiyo kwa niaba
ya Askofu Evaristus Chengula wa Jimbo Katoliki la Mbeya, Katibu wa Tume ya Haki na
Amani Jimbo la Mbeya, Sabinus Malima amelishukuru Jeshi la Polisi kwa kutambua na
kuona umuhimu wa tume hiyo ambayo imekuwa ikitoa elimu kwa waumini wake wa kanisa
katoliki kuhusu umuhimu wa haki, amani, upendo na mapatano.
Amesema Kanisa
Katoliki kupitia Tume yake ya Haki na Amani ina jukumu kubwa ambalo imekuwa ikilifanya
tangu awali la kutoa elimu kwa waumini wake na jamii kwa ujumla kuhusu faida ya nchi
kuwa tulivu na kwamba Tume inaamini kuwa bila amani na utulivu watanzania kupitia
imani zao hawataweza kupata wasaa wa kupumzika,kutulia na kuabudu na kumwamini mwenyezi
mungu.
Malima amesema nchi ama watu wanaoingia katika vita vya wenyewe kwa
wenyewe hawataweza kupata wasaa wa kuingia Makanisani ama Misikitini kwani, vita inapita
hata katika nyumba za ibada na hivyo kila kukicha na kila dakika iendayo kwa mungu
watu wanakuwa wakikaa na kuhangahikia migogoro, malumbano, vurugu, kujiokoa na makando
kando mengine ambayo hayampendezi Mwenyezi Mungu.