2013-02-19 08:54:40

Rais Shein akutana na Askofu Augustino Shao wa Jimbo Katoliki Zanzibar kufuatia mauaji ya kinyama ya Padre Evarist Mushi


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein, amepokea kwa mshtuko mauaji ya Padri Evarist Mushi na kutoa pole kwa waumini, ndugu jamaa, marafiki na wananchi wote wa Zanzibar kufuatia kifo hicho.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Mohamed Aboud ameeleza hayo Jumatatu, Februari 18, 2013 na kusisitiza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi itawasaka hadi kuwatia mikononi na hatimaye kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wale wote waliohusika na mauaji hayo.

Waziri Aboud ameyaeleza hayo wakati alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Vuga, kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein kufuatia mauaji ya Padri Evarist Mushi wa Jimbo Katoliki Zanzibar Parokia ya Mtakatifu Joseph, Shangani.

Jumapili, Dk. Shein alikutana na Askofu Augustino Shao wa Kanisa Katoliki, Jimbo la Zanzibar, huko katika Ikulu Ndogo Migombani, Zanzibar na kueleza masikitiko yake kutokana na mauaji hayo ya Padri Mushi wa Kanisa Katoliki la Zanzibar, na kuelezea haja ya kuwepo kwa uvumilivu katika kipindi hichi cha msiba.

Katika mazungumzo na waandishi wa habari, Waziri Aboud alisema kuwa Serikali imejipanga vizuri kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama ili kuhakikisha kuwa watu wote waliohusika na mauaji hayo wanakamatwa mara moja. “Kutokana na jiografia ya Zanzibar, Tunaelewa kwamba zipo sehemu katika kisiwa cha Zanzibar ambazo wahalifu wanaweza kuzitumia, hivyo Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo husika vitaziba mianya yote ili kupambana na uhalifu “, alisema Aboud.

Matendo ya uhalifu yanafanywa katika mazingira ya usiri mkubwa kwa hivyo ili wahalifu hao wakamatwe wananchi hawana budi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi pale wanapohitajika. Akijibu suali la Mwandishi, Mhe.Aboud alikanusha taarifa zilizozagaa mitaani za kuwepo silaha nyingi mikononi mwa watu wasiohusika na kuwataka wananchi kuondoa hofu.


Sambamba na hayo, Mhe. Aboud amewataka viongozi wa dini mbali mbali pamoja na waumini wa dini zote hapa Zanzibar kuwa wastamilivu katika kipindi hiki kigumu cha maombolezi. Aidha, Waziri Aboud alisisitiza haja ya kuwepo uvumilivu kwa waamini wa dini zote ili kuirejesha Zanzibar katika historia yake ya kutokuwa na migongano ya kidini.








All the contents on this site are copyrighted ©.