2013-02-19 09:25:05

Professa Mario Monti akutana na Papa Benedikto XVI


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Jumamosi, jioni tarehe 16 Februari 2013 amekutana na kufanya mazungumzo ya faragha na Professa Mario Monti, Waziri mkuu wa Italia. Hili lilikuwa ni tukio la Baba Mtakatifu kuagana rasmi na Professa Monti. Taarifa kutokana katika mkutano huu zinabainisha kwamba, mazungumzo ya viongozi hawa yamefanyika katika hali ya utulivu na amani ya ndani.

Professa Monti kwa mara nyingine tena amemshukuru Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kutokana na upendo na heshima kubwa aliyowaonesha wananchi wa Italia katika kipindi chote cha uongozi wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kanisa na Jumuiya ya Kimataifa, itaendelea kukumbuka na kuenzi mchango wake mkubwa katika maisha ya kiroho, kimaadili na utu wema.

Professa Monti anasema, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, ni kiongozi aliyeguswa kwa namna ya pekee na mahangaiko ya watu: kiroho, kimwili na kijamii. Licha ya magumu na kukengeuka kwa utu na maadili mema, bado Baba Mtakatifu anaonesha matumaini yake ya dhati kwa wananchi wa Italia na Bara la Ulaya katika ujumla wake.







All the contents on this site are copyrighted ©.