Maaskofu Katoliki wako Zanzibar kushiriki katika Ibada ya Kumwombea Marehemu Padre
Evarist Mushi!
Waamini wa Kanisa Katoliki nchini Tanzania, Jumatano, tarehe 20 Februari 2013 watakusanyika
kusali kwa ajili ya kumwombea Marehemu Padre Evarist Mushi aliyeuwawa kikatili Jumapili,
tarehe 17 Februari, 2013 wakati akienda kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu. Hii pia
itakuwa ni nafasi ya kusali kwa ajili ya kuombea amani na utulivu nchini Tanzania
kutokana na vitendo vya madhulumu ya kidini vinavyofanywa dhidi ya Wakristo.
Taarifa
kutoka Dar es Salaam zinabainisha kwamba, kuna idadi kubwa ya Maaskofu Katoliki Tanzania
wanaotarajia kuhudhuria mazishi ya Padre Evarist Mushi (55), kama kielelezo cha mshikamano
wa imani, katika kipindi hiki cha madhulumu ya kidini. Waamini na watu wenye mapenzi
mema wanasubiri kusikia tamko la Baraza la Maaskofu kuhusu madhulumu ya kidini na
uchinjaji wa nyama jambo ambalo pia limepelekea hivi karibuni mauaji ya Mchungaji
Mathew Kachira, katika Kitongoji cha Buselesele, Katoro, Mkoani Geita.
Kardinali
Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam akizungumzia juu ya mauaji
ya Padre Evarist Mushi wa Jimbo Katoliki Zanzibar anasema, hili ni tukio la kupangwa,
kwani kama vyombo vya ulinzi na usalama vingeweza kuwa makini kidogo, mauaji haya
yasingalitokea. Vipeperushi na mihadhara ya kashfa za kidini inayoendeshwa na Kikundi
cha Uamsho ni kielelezo tosha kabisa. Vyombo vya ulinzi na usalama vinafahamu kwa
hakika kile kinachoendelea nchini Tanzania.
Kardinali Pengo anasema, mauaji
ya Padre Evarist Mushi yametokea wakati anakwenda kutekeleza shughuli zake za kichungaji.
Kifo chake si tu pigo kwa Kanisa Katoliki bali ni kwa Taifa zima la Tanzania na wapenda
amani wote. Vitendo vya chokochoko na madhulumu ya kidini visipodhibitiwa kikamilifu,
Tanzania inaweza kujikuta pabaya. Jambo la msingi kwa watanzania ni kujenga na kudumisha
moyo wa uvumilivu, upendo na mshikamano wa kitaifa.
Kardinali Pengo anasema,
kuna haja ya kuombea amani na utulivu pamoja na kuelezana ukweli, utakaowaweka huru.
Askofu msaidizi Eusebius Nzigilwa wa Jimbo kuu la Dar es Salaam anatarajiwa kuongoza
Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuombea amani, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu
Yosefu, Jimbo kuu Dar es Salaam, majira ya jioni.