Tamko la Jukwaa la Kikristo mkoani Mbeya kuhusu mauaji ya viongozi wa Kikristo Tanzania
Viongozi wakuu wa Wakristo mkoani Mbeya wametoa tamko zito kwa Serikali ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania kufuatia mfulululizo wa matukio ya mauaji ya viongozi wa
dini na vurugu zinazoendana na vita ya kiimani kuwa ni matokeo ya serikali kuendelea
kukumbatia sera za udini Jukwaa la Wakristo mkoani Mbeya linaundwa na Waamini wa Kanisa
Katoliki, Baraza la Makanisa ya Kikristo Tanzania pamoja na Baraza la Makanisa ya
Kipentekoste Tanzania na kutolewa tarehe 18 Februari, 2013 mbele ya waandishi wa habari
katika ukumbi wa Kanisa la Pentekoste, Jijini Mbeya. Jukwaa la Wakristo linasema,
Serikali imelifumbia macho suala la udini na sasa madhara yake yanaanza kujionesha
kwa kasi ya ajabu!
"Ushahidi wa CD na DVD za Sheikh Ilunga ndiyo matokeo
haya lakini Serikali ni kama imebariki vitendo hivi na leo tumeshuhudia Padre Evaristi
Mushi wa Kanisa Katoliki Parokia ya Minazi Miwili Zanzibar ameuawa kwa kupigwa risasi,
Mchungaji Mathayo Kichila wa Geita aliyechinjwa, Padre wa Kanisa Katoliki Zanzibar
aliyepigwa risasi mwezi Desemba, Makanisa yamebomolewa na vitu vya thamani kuharibiwa,
lakini Serikali ipo kimya,"alisema Katibu wa Jukwaa hilo. Askofu Damianos Kongoro
wa Kanisa la Pentekoste.
Alisema kwa nini wasite kusema kwamba serikali inaibeba
dini ya Kiislamu kwa kuwa jukumu la Serikali ni kuhakikisha wananchi wote wanaishi
kwa amani na utulivu lakini haipo hivyo kwa Serikali ya awamu ya nne. Limesema sehemu
ya tamko hilo kuwa mshukiwa wa kwanza anayejuwa kila kitu ni Sheikh Ilunga aliyesambaza
CD na DVD kuhusu mikakati ya kuwauwa Wachungaji, Mapadre na Maaskofu na matokeo yake
yameanza kuonekana lakini bado yupo huru na madhara yameanza kujitokeza.
"Serikali
inatushangaza kwa viongozi wa kikristo wakiuawa na kufanyiwa vurugu inasema ni wahuni
lakini wakifanyiwa unyama viongozi wa kikristo inasema tuvumiliane wakati mchungaji
ameuawa Buserere mkoani Geita na kikundi kinachodhaniwa ni wanaharakati wa Kiislamu
wenye jazba na ghadhabu kali inayodaiwa kutokana na mvutano wa wakristo na waislamu
kuhusu nani mwenye haki kisheria kuchinja nyama, hatua zilizochukuliwa haziridhishi
wala kukidhi matakwa ya wananchi wapenda amani,"walisema.
Wametolea mifano
ya Mwenyekiti wa CCM Rungwe, John Mwankenja aliyeuawa baada ya kupigwa risasi kwa
mambo yanayodhaniwa ni ya kisiasa Serikali ilichukuwa hatua madhubuti na kutuma wachunguzi
kutoka Dar es Saalam na wananchi waliridhika na uchunguzi huo iweje kuchukulia kiurahisi
suala la viongozi wa kikristo.
"Ili wakristo wote nchini warudishe imani yao
kwa Serikali mambo yafuatayo ni lazima yachukuliwe hatua za haraka iwezekanavyo:
Serikali izingatie utawala wa sheria kulingana na ahadi yake katika kushughulikia
masuala ya kijamii na siyo vinginevyo. Suala la kuuwa lisichukuliwe kama mazoea na
inapotokea Serikali lazima ichukuwe hatua stahiki kwa kuzingatia utawala wa sheria,
tunataka serikali itueleze ni ushahidi gani zaidi inayoutaka kuliko ule uliopatikana
kwenye CD na DVD zilizotolewa na sheikh Ilunga kama kweli inazingatia utawala wa sheria,"
wamesema.
Wameongeza "tunataka serikali iwajibike kutolea ufafanuzi kauli ya
waziri wa Nchi Steven Wasira inayohusu haki ya kuchinja kwa Waislamu kama inatokana
na sheria gani ya nchi, kama serikali inatekeleza utawala wa sheria tunataka Wakristo
tuwe na machinjio na bucha zetu kulingana na imani yetu,"
Viongozi hao wamesema
kama Serikali haitachukuwa hatua za makusudi katika kutekeleza madai yao kama viongozi
wa dini ya kikristo watachukuwa hatua ya kuwaambia waumini wao kwamba Serikali inakumbatia
dini ya kiislamu na wao watajuwa la kufanya.
Hata hivyo Maaskofu hao wamesema
pamoja na kutaka utekelezaji wa haraka kutoka kwa serikali bado wamewaomba Wakristo
wawe katika hali ya maombi na utulivu kwa wakati huu ambapo wapo katika vita ya kiroho
ili Mwenyezi Mungu awaimarishie amani na utulivu, zawadi kubwa kutoka kwake na ambayo
ni nguzo ya taifa na kwamba tamko hili rasmi la Jukwaa la Wakristo mbeya lisomwe katika
makanisa yote siku ya Jumapili Febrauri, 24, 2013.
Tamko hilo limesomwa kwa
Mkuu wa Mkoa kwa naiaba ya Rais ambapo nakala zimesambazwa kwa Mwenyekiti wa CCM
Mkoa wa Mbeya,Tanzania Christian forum Taifa,Mwenyekiti wa the Tanganyika Law Society,
Wabunge wa Mkoa wa Mbeya na Vyombo vyote vya Habari mkoani Mbeya.