2013-02-18 07:47:53

Padre Evaristi Mushi auwawa kikatili Zanzibar


Rais Jakaya Mrisho Kikwete amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa ya kuuawa kwa Padri Evarist Mushi wa Parokia ya Minara Miwili, Jimbo Katoliki Zanzibar mauaji yaliyotokea Zanzibar, Jumapili tarehe 17 Februari 2013. Rais Kikwete anawapa pole nyingi na rambirambi za dhati kwa Askofu Augustino Shayo wa Jimbo Katoliki, Zanzibar, maaskofu wote nchini na waamini wote wa Parokia ya Minara Miwili kwa msiba huo mkubwa uliowakuta.
Rais kikwete amemwambia Askofu Shayo. ”Napenda kuwahakikishia kuwa tupo pamoja katika kuomboleza kifo cha Mpendwa Marehemu Padri Evarist Mushi na kuwa msiba huu ni wa kwetu sote.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Nimeliagiza Jeshi la Polisi nchini kukusanya nguvu zake zote na maarifa yake yote kuhakikisha kuwa uchunguzi wa kina na wa haraka sana unafanyika ili kubaini mhusika ama wahusika na kuwakamata ili kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria.” “Aidha, nimewaagiza Jeshi la Polisi washirikiane na vyombo vingine vya Usalama nchini na mashirika ya upepelezi ya nchi rafiki katika kufanya uchunguzi wa mauaji haya.”
Amesisitiza Rais Kikwete: “Nataka ukweli wake ujulikane ili kama kuna jambo lolote zaidi liweze kushughulikiwa na kukata mzizi wa fitina.” Vile vile, Rais Kikwete amewataka waamini wa Kanisa Katoliki na wananchi wote kuwa watulivu wakati Serikali inashughulikia suala hili na kuwa hakuna mtu wala watu ama kikundi cha watu kitachoruhusiwa kuvuruga amani ya Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.