2013-02-18 08:48:12

Madhulumu ya viongozi wa Kanisa nchini Tanzania yaanza kushika kasi ya ajabu! hatari kwa amani na utulivu wa nchi!


Askofu Augustine Shao wa Jimbo Katoliki Zanzibar anasema kwamba, hadi sasa Kanisa halijafahamu sababu zilizopelekea mauaji ya Padre Evarist Mushi na kwamba, Kanisa linasubiri kusikia taarifa za uchunguzi kutoka kwa Jeshi la Polisi nchini Tanzania. Padre Mushi ameuwawa kwa kupigwa risasi tatu wakati akiwa bado ndani ya gari lake.

Padre Evarist Mushi (55) Paroko wa Parokia ya Minara Miwili, Jimbo Katoliki Zanzibar, Jumapili tarehe 17 Februari, 2013 asubuhi, amepigwa risasi na watu wasiojulikana eneo la Mtoni Mjini Magharibi, wakati alipokuwa anakwenda kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu Kanisa la Betras. Baada ya tukio hilo Padre Mushi alikimbizwa katika Hospitali ya Mnazi mmoja, lakini baadaye alifariki dunia.

Matukio ya kuwashambulia viongozi wa kidini na uchomaji wa Makanisa Zanzibar yameendelea kujirudia rudia, kiasi cha wananchi kutokuwa tena na imani na Jeshi la Polisi, hasa kutokana na majibu rahisi na ahadi ambazo zimekuwa zikitolewa na viongozi wa Serikali kwa nyakati mbali mbali, lakini matokeo yake ni viongozi wa Kanisa kuendelea kudhulumiwa, kana kwamba, hawana haki ya kuishi na kufanya utume wao Zanzibar.

Itakumbukwa kwamba, Desemba 2012, Padre Ambrose Mkenda wa Jimbo Katoliki Zanzibar alipigwa risasi na watu wasiojulikana wakati akiwa nje ya nyumba yake, baada ya Maadhimisho ya Ibada Takatifu ya Misa. Wachunguzi wa masuala ya kidini wanasema, hivi karibuni kumekuwepo na vitisho vya wazi wazi dhidi ya wakristo Visiwani Zanzibar. Kumekuwepo na vipeperushi vinavyodai kwamba, kupigwa risasi kwa Padre Ambrose Mkenda, sio mwisho wa mapambano!

Hivi karibuni kulitokea vurugu za kidini kati ya waamini wa dini ya Kiislam na Wakristo, Buselesele Geita na kupelekea mauaji ya kiongozi mmoja wa dini. Viongozi wa Serikali ya Tanzania walikemea na kushutumu sana mauaji haya. Katika salam zake za rambi rambi wakati wa maziko ya Marehemu Askofu Thomas Laizer wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Tanzania, hivi karibuni, Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania aliwataka viongozi wa dini nchini Tanzania kuacha na kujiepusha na kauli zenye kuleta chuki na uhasama, kwani zinaweza kuleta vurugu na kuhatarisha misingi ya haki na amani.

Wachunguzi wa masuala ya kidini wanasema, haitoshi kwa viongozi wa kidini kufanya majadiliano, kwani Serikali pia inawajibika kuhakikisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao. haiwezekani watu wakaendelea kukaa kimya wakati Makanisa yanachomwa na viongozi wanauwawa kikatili.

Askofu mkuu Norbert Wendelin Mtega wa Jimbo kuu la Songea, Tanzania, aliwahi kusema kwamba, chokochoko za kidini zinazpotokea bila kuzitafutia ufumbuzi makini, wahusika watambue kwamba, wanaunda mazingira yatakayolitumbukiza Taifa katika maafa makubwa. Kuna haja ya watu kujenga na kudumisha utawala wa sheria; kukuza na kuendeleza majadiliano ya kidini, kila mtu akiheshimu na kumthamini jirani yake.

Uhuru wa kidini ni nguzo msingi wa haki nyingine zote. Historia inabainisha kwamba, chokochoko na kinzani za kidini zinaweza kusababisha maafa makubwa katika Jamii, kamwe matukio ya mauaji na uchomaji wa Makanisa yasifumbiwe macho, bali wahusika wakamatwe na kufikishwa kwenye mkondo wa sheria.

Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, Insipekta Said Mwema ametuma kikosi kazi kitakacholivalia njuga tatizo la madhulumu kwa viongozi wa kidini na uchomaji wa nyumba za Ibada, ili kuwatafuta wahusika, wakipatikana washughulikiwe kisheria ili kukata mzizi wa fitina. Wachunguzi wa haki msingi za binadamu wanasema, kauli kama hii pia ilitolewa pale Padre Ambrose Mkenda alipopigwa risasi na watu wasiofahamika. Baada ya uchunuzi wa Polisi, ikagunduliwa kwamba, "hakuna uhusiano wowote na chuki za kidini". Watanzania wengi wanasubiri kusikia ukweli na kuona haki ikitendeka.







All the contents on this site are copyrighted ©.