Jubilee ya miaka 25 ya Baraza la Maaskofu Katoliki India: waliko wa kushikamana katika
maisha na utume wa Kanisa
Baraza la Maaskofu Katoliki India, hivi karibuni limeadhimisha Jubilee ya Miaka 25
tangu lilipozinduliwa sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Imani. Kipindi chote hiki
kimekuwa ni fursa ya kuku ana kukomaa kwa kukabiliana na changamoto mbali mbali zilizokuwa
zinajitokeza katika maisha na utume wa Kanisa, daima kwa kujikita katika tunu msingi
za Kiinjili, Umoja na Mshikamano wa dhati. Ni matumaini ya Watu wa Mungu kwamba, Maaskofu
wao mahalia watawashirikisha kwa kina man’gamuzi ya Imani, Matumaini na Mapendo, kwa
njia ya ushuhuda wa maisha adili.
Wanatamani kuwaona Maaskofu wachapakazi,
wakiwa na ari na moyo wa kimissionari, tayari kujitoa kimaso maso kumtangaza Kristo
kwa ushupavu na moyo mkuu. Askofu hana budi kuwa ni kiungo thabiti katika maisha na
utume wa Kanisa, ili kuwawezesha Makleri na Waamini Walei kushirikiana kwa pamoja
katika kutangaza Injili ya Kristo sanjari na kuwahudumia maskini na wote wanaosukumizwa
pembezoni mwa Jamii. Maaskofu daima wakumbuke kwamba, Kanisa ni la Kristo mwenyewe,
amewadhaminisha: kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza Watu wa Mungu. Watu wanataka
kuona mifano bora kutoka kwa viongozi wao.
Hayo yamesemwa hivi karibuni na
Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Barza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu wakati
wa ziara yake ya kichungaji nchini India, kama mwakilishi wa Baba Mtakatifu Benedikto
wa kumi na sita katika Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 25 tangu Baraza la Maaskofu
Katoliki India lilipoanzishwa. Baba Mtakatifu anawaalika Maaskofu kujenga na kuimarisha
uhusiano wao wa dhati na Kristo kwa njia ya Sala na kwa njia hii wanaweza kuwa kweli
ni vyombo madhubuti vya Uinjilishaji, katika Mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.
Maaskofu
wajitahidi kutafuta fadhila ya hekima katika utekelezaji wa dhamana na majukumu yao
ndani ya Kanisa bila kusahau kuomba ushauri kwa masuala mbali mbali. Maaskofu wawe
na nguvu katika kutafuta mema na kuyaendeleza; wawe na ujasiri wa kukabiliana na madhulumu,
mateso hadi kifo, daima wakijitahidi kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya
Kristo, utu na heshima ya binadamu. Ukweli, uwazi na haki viwawezeshe Maaskofu kuwa
kweli ni viongozi wa Kanisa kwa kuondokana na kinzani zisizokuwa na msingi; majungu
na hata wakatimwingine upendeleo kwa baadhi ya watu.
Maaskofu wasimame kidete
kulinda na kutetea Imani ya Kanisa Katoliki. Kwa kuwa ni Walimu, wajitahidi kurithisha
Mafundisho Tanzu ya Kanisa, Liturujia na Mapokeo ya Kanisa, daima wakijitahidi kuwa
na uchaji wa Mungu. Wayafahamu Maandiko Matakatifu kwa kina na mapana, wawasaidie
waamini wao kumfahamu Yesu, ili waweze kupata uzima wa milele. Maandiko Matakatifu
yasomwe na kutafsiriwa mintarafu Mafundisho Tanzu pamoja na Mapokeo ya Kanisa. Majando
kasisi wanapokuwa katika malezi, wapewe mafundisho sahihi kuhusu falsafa na taalimungu.
Katika
Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, Kanisa pia linaadhimisha Jubilee ya Miaka 25 tangu
Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili alipochapisha Waraka wa Kichungaji kuhusu Waamini
Walei, ”Christifideles Laici”. Hili ni kundi muhimu sana katika mchakato wa kuyatakatifuza
malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao. Watambue kwamba, kwa njia ya Sakramenti
ya Ubatizo wanashiriki: ukuhani, unabii na ufalme wa Kristo. Maaskofu wajitahidi kuimarisha
na kushirikisha vyama vya kitume kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa kwani hivi
ni zawadi ya Roho Mtakatifu, lakini jambo la msingi pia ni kudumisha umoja na mshikamano
wa Familia ya Mungu katika Kanisa Mahalia. Maaskofu ni kielelezo cha umoja wa Kanisa
na kwamba, wanayo dhamana ya Kuinjilisha ulimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha
yao.
Mapadre ni wasaidizi wa kwanza wa Maaskofu katika utume wao! Ni wajibu
na dhamana kubwa kwa Maaskofu kuwa karibu na Mapadre pamoja na watawa wanaofanya nao
utume. Wawajali katika maisha na mahangaiko yao ya ndani kwa kuwasaidia kadiri ya
uwezo wa Maaskofu. Upendo, umoja na mshikamano uwe ni dira katika maisha na utume
wa Kanisa mahalia. Jubilee ya miaka 25 tangu Baraza la Maaskofu Katoliki India lilipoanzishwa,
iwe ni fursa ya kufanya tafakari ili kubainisha mafanikio, mapungufu na kujiwekea
malengo kwa siku za usoni.