Rais Otto Fernando Perez Molina akutana na Baba Mtakatifu Benedikto XVI mjini Vatican
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Jumamosi, tarehe 16 Februari 2013 amekutana
na kufanya mazungumzo na Rais Otto Fernando Pèrez Molina wa Guatemala na baadaye akakutana
na viongozi waandamizi kutoka Vatican chini ya Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu
mkuu wa Vatican. Viongozi hawa wawili katika mazungumzo yao wameridhika na uhusiano
mzuri uliopo kati ya Vatican na Guatemala.
Rais Molina amelipongeza Kanisa
Katoliki kutokana na mchango wake katika mchakato wa maendeleo endelevu nchini mwake,
hususan katika sekta ya elimu na urithishaji wa tunu msingi za kiutu na kiroho, bila
kusahau huduma za kijamii kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.
Rais amelishukuru Kanisa kwa mchango mkubwa lililotoa kwa waathirika wa tetemeko la
ardhi lililoikumba Guatemala hivi karibuni.
Viongozi hawa wawili wameonesha
umuhimu wa pande hizi mbili kuendelea kushirikiana katika harakati za kupambana na
umaskini; udhibiti wa matumizi haramu ya dawa za kulevya; vitendo vya jinai na huduma
kwa wageni na wahamiaji. Wamekubaliana kimsingi kwamba, maisha ya binadamu yanapaswa
kulindwa na kudumishwa, tangu pale mtoto anapotungwa mimba hadi mauti ya kawaida yanapomfika
kadiri ya mpango wa Mungu.