2013-02-16 10:25:16

Padre Federico Lombardi: Someni alama za nyakati!


Tamko la Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kung'atuka kutoka madarakani, ni tukio ambalo limewaacha watu wengi wakiwa wamepigwa na bumbuwazi, ndani ya Kanisa, Vatican na nje ya Kanisa lenyewe, kiasi cha watu wengi kuguswa na tukio hili muhimu sana. Ni uamuzi ambao umewashtua sana wale ambao hawamfahamu Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kwa ufasaha mkubwa wala kujitahidi kusoma alama za nyakati.

Alikwisha onesha dhana hii alipokuwa anafanyiwa mahojiano na mwandishi wa kitabu "Mwanga wa Dunia", akajibu kwa unyenyekevu na usiri mkubwa kuhusu mikakati yake ya kichungaji kwa siku za usoni, katika maelezo yake alitambua kwamba, hii ni dhamana aliyokabidhiwa kwa ajili ya mafao na maendeleo ya Kanisa na wala si kielelezo cha madaraka.

Tangu mwanzo alionesha kwamba Yeye ni mfanyakazi mnyenyekevu katika Shamba la Bwana, akajitahidi kutumia nguvu, akili, ujuzi na maarifa kutekeleza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, lakini umri pia ulikuwa unachanja mbuga!

Ni sehemu ya Tahariri ya Padre Federico Lombardi anapojaribu kuangalia tena kwa jicho la imani na matumaini uamuzi wa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita wa kung'atuka kutoka madarakani baada ya kuchunguza dhamiri yake mbele ya Mungu kwa jicho la imani na uhuru wa ndani, akambua wajibu na nguvu alizokuwa nazo kwamba, hasingeweza tena kukabiliana kwa ari na moyo mkuu dhamana aliyokuwa amekabidhiwa kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Hii ni busara ya Kibinadamu na Kikristo kwa mtu anayeishi mbele ya Mungu katika imani na ukweli, anatambua nguvu na uwezo wake na kuamua kutoa fursa ya kuliongoza Kanisa kwa Papa mwingine ili kuongeza ari na matumaini zaidi. Kuongoza Kanisa la Kristo ni dhamana nyeti si kama wanavyodhani baadhi ya watu. Kuna changamoto na matatizo makubwa yanayojitokeza ndani na nje ya Kanisa; mambo yanayohitaji nguvu ya ziada, mwelekeo mpana na mikakati makini ya shughuli za kichungaji. Padre Lombardi anasema, hili si jambo dogo!

Baba Mtakatifu hakung'atuka kutoka madarakani wakati wa shida na maguu, lakini kwa imani na matumaini anawaalika waamini kujiachilia mikononi mwa Roho Mtakatifu na Khalifa Mpya wa Mtakatifu Petro. Wakati huu anaonja sala za watu wenye mapenzi mema, wanaoendelea kumsindikiza, changamoto na kwa wengine kuungana naye katika sala ili kuimarisha uhusiano huu wa kiroho pengine kuliko ilivyokuwa kwa siku za nyuma. Huu ni mshikamano katika uhuru kamili, ndivyo anavyohitimisha tahariri yake Padre Federico Lombardi, Mkurugenzi wa Radio Vatican na Msemaji mkuu wa Vatican kwa juma hili.







All the contents on this site are copyrighted ©.