Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Ijumaa, tarehe 15 Februari 2013 alikutana
na wanachama wa Chama cha shughuli za Mtakatifu Petro, kwa mara nyingine tena, amekazia
umuhimu wa fadhila ya imani inayopaswa kuuishwa kwa njia ya matendo. Ni mwaliko kwa
waamini kuendelea kuifanyia kazi fadhila hii, ili hatimaye, iweze kukua, kukomaa na
kuzaa matunda yanayotarajiwa na kwamba, kuna uhusiano wa dhati kati ya imani na mapendo.
Baba
Mtakatifu amewakumbusha wanachama hao kwamba, imani na mapendo ni chanda na pete na
kamwe fadhila hizi haziwezi kutenganishwa, bali imani inapaswa kuoneshwa kwa njia
ya matendo ya huruma. Hiki ni kielelezo makini cha imani tendaji, imani inayojikita
katika mchakato wa kumletea mwanadamu maendeleo endelevu: kiroho na kimwili. Huduma
za kimwili zinazotolewa na Kanisa ni dhamana fungamanishi inayopania kuwashirikisha
watu ule upendo wa Kristo ambao Kanisa limeupokea na kuwagawia wengine.
Hii
ni changamoto inayotolewa na Mama Kanisa wakati huu wa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani,
kwa kuwataka waamini kuhakikisha kwamba, waamini wanakutana na Kristo anayewaletea
mabadiliko katika hija ya maisha yao ya kiroho, ili hatimaye, kutolea ushuhuda wa
maana ya upendo wa Kikristo. Matendo ya huruma wakati huu wa Kipindi cha Kwaresima
ni hatua inayomwezesha mwamini kumwendea Kristo na Kristo kumwendea mwanadamu.
Baba
Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anawatakia wanachama wa Chama cha shughuli za
Mtakatifu Petro, kuendelea kuimarika wanapofanya hija yao ya kiroho kwenye Kaburi
la Mtakatifu Petro. Iwe ni fursa ya kukuza na kuimarisha neema ya ubatizo, daima wawe
na ari na moyo wa kutaka kutolea ushuhuda wa imani tendaji katika hija ya maisha yao
ya kila siku.
Wanachama hawa kwa upande wao, wamemhakikishia Baba Mtakatifu
kwamba, wataendelea kuchangia kwa hali na mali shughuli za matendo ya huruma zinazofanywa
na Khalifa wa Matakatifu Petro, kama kielelezo cha upendo na mshikamano unaoonesha
ile furaha ya imani kwa Kristo na Kanisa lake. Kwa njia ya imani wanaweza kuwaonjesha
jirani zao maskini na wahitaji ile sura ya Kristo mfufuka.
Ndiyo maana, kile
kidogo walichojinyima wanakiweka mikononi mwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, ili kiweze
kuwafariji wale wanaohitaji zaidi. Wanamshukuru kwa unyenyekevu na ujasiri mkubwa
katika kulihudimia Kanisa la Kristo.