Maaskofu Katoliki kutoka Mashariki ya Kati wanamshukuru Baba Mtakatifu Benedikto wa
kumi na sita kwa kuwa bega kwa bega na Kanisa Mashariki ya Kati, nyakati za shida
na magumu, daima akiwahimiza kujisikia kuwa ni sehemu ya Kanisa na kwa ajili ya Kanisa
na kwamba, walikuwa wanalo jukumu la kusonga mbele kwa imani na matumaini bila ya
kukatishwa tamaa na magumu wanayokabiliana nayo katika kuwahudumia Watu wa Mungu,
huko Mashariki ya Kati.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwa mara
nyingine tena ameonesha ukweli, busara na unyenyekevu wa hali ya juu kwa kutamka kwa
utashi na uhuru kamili kwamba, anang'atuka kutoka madarakani. Maaskofu kutoka Mashariki
ya Kati wanamshukuru na kumpongeza wanasema, wataendelea kumsindikiza katika awamu
ya pili ya maisha yake kwa njia ya sala.
Ni kiongozi ambaye amesimama kidete
kulinda na kutetea: haki na amani; utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura
na mfano wa Mungu. Ameng'atuka kutoka madarakani si kwa kushinikizwa kama ambavyo
baadhi ya watu wanataka kuwasadikisha watu wengine, bali kutokana na upendo na mafao
ya Kanisa.
Ni mfano ya mfanyakazi mnyenyekevu katika Shamba la Bwana anayetambua
uwezo wake, kiasi hata cha kudiriki kuachia dhamana yake kama kiongozi mkuu, ili kutoa
nafasi kwa kiongozi mwingine mwenye nguvu, ari na kasi kubwa zaidi kuendeleza utume
wa Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Maaskofu Katoliki Mashariki wanamshukuru Baba
Mtakatifu kwa kuitisha, kuadhimisha na hatimaye, kuwapatia Waraka wa Kichungaji, Kanisa
Mashariki ya Kati, "Ecclesia in Medio Oriente". Ni Sinodi iliyopania kujenga na kuimarisha
misingi ya haki, amani, upendo na utulivu kwa kutambua kwamba, wote ni watoto wa Mungu
na tofauti zao ziwe ni kichocheo cha kushikamana na wala si kwa ajili ya kuwagawa!
Wananchi wanaoishi Mashariki ya Kati wanapaswa kujikita katika mchakato wa haki, amani
na upatanisho. Waamini waendelee kutolea ushuhuda wa imani katika matendo.
Maamuzi
yaliyofanywa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, yataendelea kuwa rejea kwa
watu waliopewa dhamana ya uongozi ndani ya Kanisa na Jamii kwa ujumla, kuchunguza
dhamiri zao kwa unyenyekevu mbele ya Mwenyezi Mungu na kuangalia jinsi wanavyotekeleza
majukumu yao ikiwa ni kadiri ya mapenzi ya Mungu au ni kwa kujitafuta wao wenyewe
na masilahi na utukufu binafsi.
Viongozi wajifunze kutafuta mafao ya wengi
wanapotekeleza wajibu na dhamana yao ndani ya Jamii. Viongozi watambue kwamba, wamepewa
wajibu wa kuhudumia na wala si kuhudumiwa!