Watanzania Roma watoa heshima zao kwa Ibada ya Misa ya wafu kwa Marehemu Alphonsina
Shayo.
Alhamisi hii majira ya saa tano za asubuhi , Watanzania Roma walishiriki katika Ibada
ya Misa ya Wafu kwa nia ya kutoa heshima zao za mwisho na kuiombea Roho ya Marehemu
Alphosina Anselmi Shayo, aliyefariki hapa Roma wiki iliyopita.
Ibada hiyo,
iliyofanyika katika Parokia ya Mtakatifu Dorothea, ikiongozwa na Padre Felix Mushobozi
wa Shirika la Damu Takatifu ya Yesu , akishirikiana na Mapadre wengine ya kadhaa,
pia ilihudhuriwa na makumi ya Masista wa mashirika mbalimbali na walei kadhaa akiwepo
mwakilishi wa Ubalozi Bwana Mbilinyi.
Marehemu Alphosina alifaki dunia , Mapema
Alhamis 6 Februari 2013, baada ya kupita muda wa saa kadhaa, tangu alipowasili Roma
Jumatano, akitokea Arusha Tanzania, kwa lengo la kushiriki katika sherehe ya kuweka
nadhiri za daima, mdogo wake, Sista Maria Blanca Shayo. Sherehe iliyofanyika Siku
ya Jumamosi 9 Feburari 2013. Sherehe iliyomhusu pia Sista Maria Basilisa Puka, wote
wawili wakiwa ni Masista wa Shirika la Sakramenti Takatifu, wazawa wa Moshi Tanzania.
Kifo cha Alphonsina Shayo, kimebaki kuwa kitendawili.
Padre Felix Mushobozi
katika homilia yake, ametahadharisha, hakuna anayejua wakati wala mahali, au kwa namna
gani kifo kitamfika au kuepushwa nacho isipokuwa Mungu peke yake. Ametahadharisha
kifo hakijali hadhi, cheo, umri wala jenda. Hivyo basi, kila kinapotokea, unakuwa
ni mwaliko mpya kwa walio hai, kuwa tayari, wakati wowote, tunapoitwa kuhitimisha
hija ya maisha duniani.
Nae kiongozi wa Jumuiya ya wanafunzi Katoliki Roma,
alitoa shukurani zake za dhati kwa ushirikiano mzuri ulioonyeshwa na Watanzania tangu
Msiba huu ulipotokea. Wengi wameshiriki kwa namna moja au nyingine kupitia sala,
faraja na rambirambi na kusaidia katika kufanikisha taratibu za mwili wa Marehemu
kurudishwa nyumbani. Amesema mshikamano na umoja huu uzidi kuwa ngao na utambulisho
wa Watazania mahali popote walipo.
Mara baada ya Ibada hii, Mwili wa Marehemu
Alphonsina ulipelekwa Uwanja wa Ndege wa Roma , tayari kwa kusafirishwa mapema Ijumaa
hadi Tanzania.Marehemu ameacha Mme na watoto wawili. Tunamwombea pumziko la Milele,
Amina.