Waamini nchini India tarehe 22 Februari: Siku kuu ya Ukulu wa Mtakatifu Petro, kumuenzi
Baba Mtakatifu kutokana na mchango wake mkubwa kwa Kanisa!
Katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Ukulu wa Mtakatifu Petro, inayofanyika kila Mwaka
ifikapo tarehe 22 Februari, Baraza la Maaskofu Katoliki India, limeamua kwa Mwaka
huu, kumuenzi Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kama njia ya kutambua mchango
wake katika kutetea: maisha, utu na heshima ya binadamu.
Ni kiongozi aliyetoa
changamoto ya pekee katika kukuza na kuendeleza majadiliano ya kidini na kiekumene
sanjari na kukabiliana na changamoto za ukanimungu, athari za utandawazi na mmong'onyoko
wa kimaadili Barani Asia, kwa kukazia umuhimu wa Mafundisho Jamii ya Kanisa.
Waamini
na wananchi wenye mapenzi mema nchini India, watatumia muda wa saa moja kwa ajili
ya kuabudu Ekaristi Takatifu, kwa ajili ya kumwombea Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi
na sita, ambaye hivi karibuni kwa utashi na uhuru kamili ameamua kung'atuka kutoka
madarakani. Amekuwa mstari wa mbele kukoleza majadiliano ya kitamaduni, akiwahamasisha
waamini na watu wenye mapenzi mema kujitoa kimaso maso kuwasaidia maskini na wahitaji
kwa njia ya mshikamano wa upendo.
Kardinali Oswald Gracias, Rais wa Baraza
la Maaskofu Katoliki India ambaye pia ni Katibu mkuu wa Shirikisho la Mabaraza ya
Maaskofu Katoliki Barani Asia (FABC), anasema, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na
sita, ameonesha njia ya kuweza kukabiliana na changamoto mbali mbali katika uchumi,
utandawazi, utunzaji bora wa mazingira pamoja na kukabiliana fika na misimamo mikali
ya kiimani, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Mwenyezi Mungu na pili kwa maisha,
utu na heshima ya binadamu.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, licha
ya vikwazo na changamoto mbali mbali, alijitahidi kujenga jukwaa la majadiliano ya
kidini Barani Asia, kwa kutumia vyema vipaji na karama ambazo amekirimiwa na Mwenyezi
Mungu. Katika kudumisha amani, kuna haja kwa waamini na watu wenye mapenzi mema anasema
Kardinali Gracias kufanya rejea kwa ujumbe wa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na
sita katika Maadhimisho ya Siku ya Amani Duniani kwa Mwaka 2011, aliposema, uhuru
wa kidini ni nyenzo muhimu katika ujenzi wa amani duniani.
Mwaka 2012, Baba
Mtakatifu anawahimiza watu kuwa ni wajenzi wa amani na kwamba, amani si tu hali ya
kukosekana kwa vita, bali amani inafumbata pia haki na upendo.