Vijana nchini Brazil wanachangamotishwa na Baba Mtakatifu kujitosa kweli kweli kuwatangazia
wenzi wao Injili inayokoa!
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita amewaandikia Maaskofu Katoliki Brazili wakati
huu wa Kampeni ya Kwaresima kwa Mwaka 2013 inayoingia katika maadhimisho ya miaka
hamsini tangu ilipoanzishwa.
Anasema, Kipindi cha Kwaresima ni muda muafaka
wa kusali, kutubu na kufanya matendo ya huruma kama njia mahususi ya kujiandaa kikamilifu
katika maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo, kwa
kujielekeza zaidi katika maandalizi ya Siku ya Vijana Duniani, itakaofanyika mjini
Rio de Janeiro kuanzia tarehe 23 hadi tarehe 28 Julai 2013. Kauli mbiu inayoongoza
maadhimisho haya ni udugu na vijana, kama changamoto kwa vijana nchini Brazil kujitosa
kimaso maso kuitikia wito kutoka kwa Mwenyezi Mungu, wakisema bila kusita, “mimi hapa
Bwana, nitume” kama alivyosema Nabii Isaya.
Baba Mtakatifu anasema, anapenda
kujiunga na Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil, kwa kuwapatia baraka na neema kwa
wadau wote wanaojitoa bila ya kujibakiza ili kufanikisha Kampeni hii ya Kipindi cha
Kwaresima, kama sehemu ya mchakato wa kuwawezesha vijana kuwa wajenzi wa Jamii inayosimikwa
katika haki na udugu mintarafu kweli za Kiinjili. Alama za nyakati zinajionesha ndani
ya Kanisa na Jamii kwa ujumla kwa njia ya vijana, ikiwa kama fursa hizi zinazojitokeza
hazitaweza kutumiwa kikamilifu, Kanisa na Jamii inaweza kupoteza fursa ya kuleta wongofu
wa ndani. Vijana ni tumaini la leo na kesho iliyo bora zaidi.
Baba Mtakatifu
anasema, Kanisa linapenda kuwaona vijana wakishiriki kikamilifu katika maisha na utume
wa Kanisa kwa njia ya Jumuiya zao, hali wakionesha matumaini waliyo nayo ndani mwao
kwa Kanisa. Dhamana hiii nyeti inawahitaji viongozi na walezi wanaotoa kipaumbele
cha kwanza kwa katika majiundo ya vijana, wakiwaonesha dira na njia ya kufuata bila
ya kuwawekea vikwazo; wajenge mshikamano wa dhati, kwa kushuhudia kwamba: wokovu na
imani pamoja na ufuasi wa Yesu Kristo ni mambo yanayorutubishwa kila siku ya maisha.
Vijana
nchini Brazil wanahamasishwa na Baba Mtakatifu kutafuta maana ya maisha yao kwa njia
ya tafakari ya Injili ya Yesu Kristo, kwa kujenga urafiki, ili hatimaye, kujipatia
kile kilicho bora na kinachoweza kuwaokoa kutoka katika utumwa wa dhambi na mauti
kama Mwenyezi Mungu alivyomsafisha Nabii Isaya kwa kaa la moto, akawa safi, tayari
kujitosa kimaso maso kutangaza Neno la Mungu.
Vijana wanapokutana na Mwenyezi
Mungu katika hija ya maisha yao, wanapata fursa ya kuonja mabadiliko ya ndani, kiasi
hata cha kuweza kujitokeza kwa ajili ya kuwatangazia vijana wenzao Habari Njema ya
Wokovu; kugundua Jangwa na utupu wa maisha ya kiroho unaowaandama vijana wa kizazi
kipya, ili hatimaye, waweze kupokea yale mambo ya msingi tu!
Injili na Imani
ya Kanisa ni mambo muhimu sana yaliyojadiliwa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa
Vatican, kama inavyobainisha pia Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki. Vijana waonje
ile furaha ya kumwamini Kristo; wamfuate katika hija ya maisha yao, hali wakimtolea
ushuhuda katika hali mbali mbali wanamoishi, ili kuweza kutangaza utajiri wa imani
kwa Kristo na Kanisa lake. Baba Mtakatifu, anawatakia kheri na baraka wananchi wa
Brazil, lakini zaidi vijana wa kizazi kipya, akiwaweka chini ya ulinzi na usimamizi
wa Bikira Maria wa Aparecida.