2013-02-15 15:47:09

Umati wa Watanzania washiriki maziko ya Askofu mstaafu Msarikie


Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania, Alhamisi, Februari 14, 2013 ameungana na mamia kwa mamia ya waamini wa Jimbo Katoliki la Moshi na kutoka sehemu nyingine nchini, kumzika Askofu Mstaafu Amedeus Peter Msarikie. Rais Kikwete amewasili kwenye Kanisa Kuu la Kristo Mfalme, Jimbo Katoliki Moshi kiasi cha saa sita na dakika tano mchana kuungana na Marais wastaafu Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa na mamia kwa mamia wananchi kwa ajili ya mazishi ya Askofu Msarikie ambaye alifariki dunia Alhamisi iliyopita, Februari 7, 2013 kwa ugonjwa wa saratani katika hospitali moja mjini Nairobi, Kenya.

Mara baada ya kuwasili, Rais Kikwete ametia saini kwenye kitabu cha maombolezo na ikaanza ibada ya mazishi ilivyohudhuriwa na mamia kwa mamia ya wananchi wakiwamo maaskofu zaidi ya 20 kutoka majimbo mbali mbali ya Kanisa Katoliki nchini. Mwili wa Marehemu Msarikie uliteremshwa kaburini kiasi cha saa saba na dakika 35 ndani ya Kanisa hilo na Rais Kikwete akaweka udogo kwenye kaburi na baadaye shada la maua.

Akizungumza kwenye mazishi hayo, Rais Kikwete amemwelezea Askofu Msarikie ambaye alikuwa Askofu wa Jimbo la Moshi kwa miaka mingi kama “kiongozi shupavu wa kiroho ambaye aliwalea vyema Kondoo wa Bwana. Lakini pia alikuwa kiongozi hodari kwa maendeleo ya jamii yaliyowanufaisha waumini wake na hata wale wa madhehebu na dini nyingine.” Amesisitiza Rais Kikwete: “Kwa kweli sote tumepoteza mtu muhimu.

Tunamfahamu marehemu Baba Askofu Msarikie kwa mema mengi aliyowatendea watu wa jimbo lake, ya kiroho na ya maendeleo. Mimi binafsi, wana-moshi na Watanzania kwa ujumla tutamkumbuka na kumuenzi Baba Askofu Msarikie kwa mema mengi aliyowafanyia wanadamu wenzake na nchi yetu.”








All the contents on this site are copyrighted ©.