Matunda ya Jubilee ya Miaka 100 ya Chuo cha St. Albert, India
Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu
wakati wa ziara yake ya kichungaji nchini India, ameshiriki pia katika Maadhimisho
ya Jubilee ya Miaka 100 tangu Chuo cha Albert kilichoko Ranchi, kilipoanzishwa. Katika
kipindi chote hiki, kimebarikiwa kupata Mapadre: 2000; Maaskofu na Maaskofu wakuu
35 pamoja na Kardinali mmoja.
Hiki ni kati ya vyuo maarufu sana vinavyotoa
majiundo makini, Kaskazini mwa India. Kimekuwa mstari wa mbele katika kuwaandaa wadau
wa uinjilishaji nchini India, watu ambao wamekuwa msaada mkubwa katika mikakati na
shughuli za Uinjilishaji na utamadunisho, ili kuhakikisha kwamba, viongozi wa Kanisa
wanafahamu fika tunu msingi za kitamaduni na Kiinjili, ili kuweza kutekeleza barabara
majukumu yao ya kichungaji.
Hii ndiyo dira ya Kanisa katika mikakati ya majiundo
kwa Majandokasisi pamoja na kuhakikisha kwamba, Seminari na nyumba za malezi zinapata
walezi makini, wenye sifa na vigezo vinavyohitajika kwa ajili ya majiundo ya viongozi
wa Kanisa kwa sasa kwa siku za usoni.
Waseminari wanapaswa kujifunza pamoja
na kukuza ari na moyo wa kimissionari, tayari kujitoa kimasomaso kutangaza Injili
ya Kristo hadi miisho ya dunia. Watambue kwamba, wanapaswa katika maneno na matendo
yao kuwa ni Kristo mwingine kwa wale wanaowahudumia. Viongozi wa Kanisa wajitahidi
kusoma alama za nyakati, kwani dunia inabadilika kwa kasi ya ajabu!
Kardinali
Filoni katika hotuba yake kwa Waseminari chuoni hapo anakazia kwamba, Mwaka wa Imani
uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, uwasaidie
kumfahamu, kumpenda na kumhudumia Kristo, aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika
wafu; utume ambao wanapaswa kuutekeleza kwa ari na moyo mkuu, daima wakijitahidi kuwa
ni watu wa imani.
Waonje na kuguswa na mifano iliyotolewa na Mababa wa Imani
wanaosimuliwa katika Maandiko Matakatifu. Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu pamoja
na Mitume ni vielelezo makini sana vya imani katika maisha na utume wa Kanisa.
Kipindi
cha malezi kiwasaidie kunoa akili na mioyo yao barabara, tayari kuwatumikia Watu wa
Mungu bila kujibakiza. Ili kufanikisha azma hii, kuna haja kwanza kabisa kuwani watu
wa Sala wanaofanya tafakari ya kina kuhusu Neno la Mungu pamoja na kushiriki Sakramenti
za Kanisa, kwa namna ya pekee, Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho. Kipindi
cha majiundo kitumike vyema ili kujipatia ujuzi na maarifa yatakayowasaidia kutekeleza
shughuli zao za kichungaji kwa siku za usoni.
Kardinali Filoni anawaalika
Majandokasisi: kutambua na kuthamini kwa namna ya pekee fadhila ya utii, useja na
ufukara wa Kiinjili kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Ufalme wa Mungu. Maisha ya
Sala na Sadaka yawawezeshe kuvuka vikwazo, majaribu na vishawishi kwa kukimbilia daima
huruma ya Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho.
Familia ya Mungu inahitaji
viongozi waaminifu, waadilifu, wachapa kazi na wachamungu, wanaoonesha ushuhuda wa:
imani, matumaini na mapendo katika uhalisia wa maisha. Uhuru wa ndani, uwajengee moyo
wa upendo na mshikamano kwa ajili ya huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni
mwa Jamii.