2013-02-15 15:20:05

Jengeni mshikamano wa upendo na udugu kwa kushirikishana karama na rasilimali mlizokirimiwa na Mungu!


Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013 yatakayofanyika huko Rio de Janeiro, kuanzia tarehe 23 Julai hadi tarehe 28 Julai 2013, ni kipimo cha shughuli na mikakati ya kichungaji ya Maaskofu Katoliki nchini Brazil, yanayojionesha hata katika Kampeni ya umoja na mshikamano wa kidugu inayofanywa kwa Mwaka 2013 katika Kipindi cha Kwaresima.

Hii ni fursa kutoka kwa Maaskofu Katoliki Brazil, kutoa mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kushirikishana rasilimali walizo nazo kwa ajili ya mafao, ustawi na maendeleo ya ndugu zao wenye kuhitaji zaidi kuliko wao wenyewe! Itakumbukwa kwamba, Kampeni ya umoja na mhikamano wa kidugu kwa Mwaka 2011 ilijikita katika utunzaji bora wa mazingira na umuhimu wa kuendeleza elimu ya mazingira ili kumwezesha mwanadamu kupata utilimifu wa maisha yake.

Mwaka 2012, Maaskofu wakaelekeza Kampeni yao kuhusu afya kama haki msingi ya binadamu. Mwaka 2013 kampeni hii inajikita katika mwaliko kwa waamini kuonesha mshikamano wa dhati na vijana; hasa wakati huu, Kanisa linapoendelea kufanya maandalizi kwa ajili ya kuwapokea na kuwakirimia vijana watakaoshiriki katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013.

Kampeni ya umoja na mshikamano wa kidugu kwa Mwaka 2014, utakuwa ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuonesha mshikamano wa dhati kwa kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya kila mtu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Maaskofu Katoliki nchini Brazil wanaendelea kuwahamaisha vijana kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, wakiwa daima tayari kuitikia kwa maneno ya Nabii Isaya wakisema, “Mimi hapa, Bwana Nitume”. Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika ujumbe wake kwa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013, anawahamasisha vijana hawa kuwa ni wamissionari miongoni mwa vijana wenzao, daima wakijitahidi kuwa ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa.

Vijana wakuze ndani mwao, ari na hamu ya kutaka kuwa ni vyombo vya Uinjiliushaji, kwa kujitoa kimasomaso kumtumikia Mungu na jirani katika maisha ya Kipadre na Utawa.

Mada ya vijana kuongoza Kampeni ya umoja na mshikamano wa kidugu, inakuja tena kwa nguvu na kasi kubwa zaidi baada ya takribani miaka ishirini na moja, kunako Mwaka 1992, vijana walipoalikwa kwa namna ya pekee kuanza hija ya maisha ya imani, wakiwashirikisha wengine tunu msingi za maisha ya kiroho, kimaadili, kiutu na kijamii, kama alivyobainisha Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa pili katika tukio hili.

Vijana wanachangamotishwa kuyatakatifuza malimwengu katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Ili kufanikisha dhamana hii, Kanisa linawajibika kuandaa mikakati ya kichungaji, itakayowasaidia vijana kujitambua na hatimaye, kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Vijana wasaidiwe kuifahamu na kuimwilisha imani yao kwa Kristo na Kanisa lake; kwa njia ya majiundo makini ya Katekesi; Mafundisho Tanzu ya Kanisa; Biblia pamoja na Mafundisho Jamii ya Kanisa.

Vijana wanapaswa kufahamu kweli za Kiinjili na Kimaadili, tayari kuzifanyia kazi katika medani mbali mbali za maisha, kama njia yao ya ushiriki katika mchakato unaopania kuyatakatifuza malimwengu, ili ulimwengu uweze kuwa kweli ni mahali pazuri zaidi pa kuishi, watu wakiheshimiana, kuthaminiana na kusaidiana kama watoto wateule wa Mungu.

Changamoto hii bado ni hai miongoni mwa ulimwengu wa vijana hasa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimsiha Mwaka wa Imani, sanjari na kumbu kumbu ya Miaka ishirini tangu Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki ilipochapishwa kwa mara ya kwanza na Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili. Kanisa linapania kupembua kwa umakini mkubwa, ulimwengu wa vijana ili kubainisha: utajiri na mapungufu ambayo vijana wanapaswa kuyaangalia kwa umakini mkubwa vinginevyo wanaweza kujikuta wamemezwa na malimwengu na hapo kutakuwa ni patashika nguo kuchanika!

Kampeni hii imezinduliwa rasmi hapo tarehe 13 Februari 2013, Jumatano ya Majivu, Mama Kanisa anapoanza Kipindi cha Kwaresima, Siku Arobaini za: Kufunga, Kusali, Kutafakari na Kufanya Matendo ya Huruma. Kampeni ya Kwaresima, ilianzishwa kunako mwaka 1962, changamoto ya Mtaguso mkuu wa Pili wa vatican na kwa mara ya kwanza Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil, wakaanza kuadhimisha kwa mara ya kwanza kunako mwaka 1964.

Ni fursa makini inayotoa mwaliko kwa kuishi kikamilifu kipindi cha Kwaresima, kwa kufanya toba na kuchuchumilia wongofu wa ndani kama sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, yaani, mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Kampeni hii inajionesha kwa namna ya pekee katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa: Katika Ibada ya Misa Takatifu, Njia ya Msalaba na Tafakari za Neno la Mungu. Waamini wanaalikwa, kuona changamoto zinazowazunguka katika Jamii yao na kuzipima kwa mwanga wa Injili na kutekeleza kadiri ya maelekeo ya toba na wongofu wa ndani.

Familia yote ya Mungu nchini Brazil, inaalikwa kushiriki katika utume huu sanjari na kuwaonjesha jirani zao, yale matunda ya sadaka na kujinyima kwao. Maaskofu Katoliki Brazil, wamekuwa wakijadili mada mbali mbali kama vile: baa la njaa duniani; ukosefu wa fursa za ajira pamoja na matumizi haramu ya dawa za kulevya. Tema zote hizi zimewasaidia waamini kuku ana kukomaa katika maisha yao ya kiroho na kimwili.








All the contents on this site are copyrighted ©.